Mbunge wa Mbeya Mjini 'Sugu' na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga wamemkataa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite wakidai hawana imani naye katika mwenendo wa kesi hiyo.
Sugu na Masonga wanashtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli wanayodaiwa kuitoa Desemba 30,2017.
Washtakiwa leo Alhamisi Januari 25,2018 asubuhi wamefika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa ajili ya kuanza kutoa ushahidi baada ya upande wa Jamhuri kukamilisha na kufunga ushahidi wao.
Upande wa Jamhuri umewasilisha mashahidi watano mahakamani na vielelezo viwili ikiwamo sauti iliyorekodiwa.
Baada ya utaratibu wa kimahakama kukamilika ili kuanza ushahidi, wakili Boniface Mwabukusi anayewawakilisha Sugu na Masonga alimuomba hakimu Mteite akisema wateja wake wana jambo la kuieleza Mahakama.
Hakimu alipowaruhusu kuzungumza, Sugu ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, amesema kutoka ndani ya nafsi yake ameitafakari kesi na mwenendo wake na kufikia uamuzi wa kumkataa hakimu kwa kuwa hana imani naye kwa sababu tatu.
Amesema, “Naomba niitaarifu Mahakama hii kwamba nimetafakari mwenendo wa kesi hii, mimi mshtakiwa wa kwanza Joseph Mbilinyi naona nikukatae wewe hakimu kutokana na mambo yafuatayo: kwanza; sijawahi kuona hakimu yuko biased (wenye upendeleo) kama ulivyo wewe, ulivyoninyima dhamana bila sababu za kisheria na Katiba.”
“Pili, jana nimeshuhudia kielelezo cha tape recorder kikitokea mikononi mwa wakili wa serikali ambacho wakili wangu (Mwabukusi) alikikana na ukamshambulia sana wakili wangu kwamba wakati anakitoa yeye (wakili) alikuwa ametoka wakati mimi nilikuwa hapa sikuona. Sasa kitendo kile naona wewe hakimu una interest (masilahi) dhidi yangu,” amesema.
Sugu amesema, “Lakini pia jana ulikiri kwamba katika kesi hii unapata mateso, hivyo mimi ni Mkristo, sasa ili nisikupe tabu na mateso naomba nikukatae na apangiwe hakimu mwingine atakayeendesha kesi hii kwa uhuru na haki.”
Amesema kwa sababu hizo anaomba amkatae hakimu huyo.
Baada ya ombi hilo la Sugu, hakimu Mteite alimpa nafasi Masonga ambaye pia alimkataa akitoa msimamo unaofanana na wa Sugu.
Katika sababu zake, Masonga amesema, “Mheshimiwa jana ulipotoa uamuzi wa kupokea vielelezo kutoka kwa upande wa Jamhuri, wa tape recorder na register mheshimiwa hakimu ulieleza Mahakama yako kwamba unaruhusiwa kisheria wakati upande wa Jamhuri ulikubali ushahidi upokewe kama Id (utambulisho) lakini register ipokewe kama kidhibiti. Lakini bado uamuzi wako ulikuja tofauti na upande wa Jamhuri.”
Amesema, “Ulipofanya uamuzi wakati tulipokuomba dhamana, ulisema unakubaliana na hoja za pande zote mbili (utetezi na Jamhuri). Na Jamhuri walisema kwa ajili ya usalama wetu (washtakiwa), wanaomba tusipewe dhamana. Na wewe katika uamuzi wako umezingatia hoja zao lakini umezingatia zetu kwa sababu ni haki yetu kisheria na kikatiba. Na uamuzi wako ulisema unazuia dhamana kwa sababu unataka kesi hii iendee haraka, bila kujadili hoja zilizoletwa mbele yako.”
Hakimu Mteite amesema amezingatia hoja hizo na atatoa uamuzi baada ya saa moja.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment