NEC Yatoa Maamuzi Ya Rufaa Ya Mgombea Ubunge wa CHADEMA Na Rufaa 5 Za Wagombea Udiwani

MAAMUZI YA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI KUHUSU RUFAA MOJA YA MGOMBEA UBUNGE NA RUFAA TANO ZA WAGOMBEA UDIWANI

Kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 40(6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, ikisomwa pamoja na Kanuni za 34 na 35 za Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015, Tume ilipokea Rufaa moja (1) kutoka kwa Mgombea Ubunge Jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) akipinga maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo kuhusu pingamizi alilomuwekea Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Aidha, kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, ikisomwa pamoja na Kanuni za 28 na 29 za Kanuni za Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2015, Tume ilipokea Rufaa tano (5) za Wagombea  Udiwani  kutoka katika Kata ya Isamilo – Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wakipinga Maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo.  Rufaa tatu (3) ni za wagombea walioondolewa kwenye kugombea ili warejeshwe na Rufaa mbili (2) zinaomba Tume itengue uteuzi wa mgombea Udiwani aliyeteuliwa katika Kata hiyo.

Katika kikao chake cha kawaida kilichofanyika tarehe 26 Januari 2018 siku ya Ijumaa, Tume ilipitia Rufaa hizo na kuamua kama ifuatavyo:

Mosi, kuhusu Rufaa ya Mgombea Ubunge, Tume imekubaliana na maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi na hivyo Mgombea aliyekatiwa Rufaa wa CHADEMA anaendelea kuwa mgombea wa Ubunge Jimbo la Kinondoni.

Pili, kuhusu Rufaa za Wagombea Udiwani Kata ya Isamilo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, kupinga kuondolewa kugombea Udiwani katika Kata hiyo, Tume imewarejesha kuwa Wagombea Udiwani wawili wa vyama vya CHADEMA na CUF.

Tatu, Tume imekubaliana na maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi ya kumuondoa katika orodha ya wagombea Udiwani mgombea wa Chama cha UDP. Hivyo hatakuwa mgombea katika kata hiyo

Nne, Tume imekataa rufaa mbili zilizokuwa zinapinga uteuzi wa mgombea wa CCM aliyeteuliwa katika Kata hiyo na hivyo, mgombea wa CCM anaendelea kugombea Udiwani katika kata husika.

Taarifa rasmi za maamuzi ya Tume zimetumwa kwa Wasimamizi wa Uchaguzi ili wawapatie wahusika maamuzi hayo.

Kailima, R.K
MKURUGENZI WA UCHAGUZI


from MPEKUZI

Comments