Mtulia : Nilifanya Maamuzi Ya Kiume Kuhama CUF....Hivi Sasa Hadi Namba ya Rais Ninayo

Mgombea wa Jimbo la Kinondoni kupitia CCM, Maulid Said Mtulia amesema amefanya maamuzi ya kiume ya yeye kuhamia chama hicho kwa sasa kwa maana wapo wengi wanataka kufanya hivyo lakini wameshindwa kwa madai wanasubiri kulipwa kiiunua mgongo.

Mtulia ameeleza hayo wakati alipokuwa anaendelea kujinadi kwa wananchi wa jimbo la Kinondoni ambalo hapo awali alikuwa analishikilia yeye kupitia chama chake cha CUF kabla ya kujivua uanachama wake na kuenda kumuunga mkono Rais Magufuli katika jitihada zake za kuijenga nchi.

"Kujiuzulu Ubunge sio mchezo, nimefanya maamuzi ya kiume maana kuna wenzangu wengine mpaka sasa hawawezi kutoka kwa sababu wanasubiri kiiunua mgongo. Sasa kijana kama mimi nikae pale nisubirie kiunua mgongo hivi kweli ntaweza kuishi kwa kusubiri kiiunua mgongo", alisema Mtulia.

Aidha, Mtulia amesema amejinusuru kwa mengi kukihama chama chake cha awali ili aweze kuwapigania wananchi wa jimbo hilo kwa maana hapo awali alikuwa anashindwa kuyafanya majukumu yake vizuri kutokana na mgawanyiko ndani ya chama chao.

"Wenzangu Wabunge 10 walifukuzwa uanachama CUF hamkujua, mlisubiri nifukuzwe au mna roho mbaya na mimi. Hivi nilipo hapa nimeruka kwa kujinusuru nashukuru nipo salama na nimesimama tena kwa wana kinondoni ninaomba kugombea Ubunge nyie mnanuna kitu gani au huo ndio usaliti. Lakini jambo jingine mimi nimekuja CCM kwa sababu nampenda Magufuli balaah", aliuliza Mtulia.

Pamoja na hayo, Mtulia aliwashangaza baadhi ya watu kwa kusema ametumikia Ubunge ndani ya miaka miwili na kushiriki vikao vyote vya Bunge lakini hakuweza kuwa na namba ya Rais Magufuli.

"Leo ninawaambia siri yangu, nilivyokuwa Mbunge miaka miwili namba ya Rais Magufuli sikuwa nayo lakini sasa namba ninayo. Hivyo wanakinondoni mnataka nini kama mnataka maendeleo ndio haya", alisisitiza Mtulia.

Kwa upande mwingine, Mtulia amewaambia wananchi wa Jimbo la Kinondoni endapo watamchagua yeye katika chaguzi hizo za marudio zilizopangwa kufanyika mapema Februari 17 mwaka 2018 basi watakuwa wametengeneza daraja la kujipatia maendeleo.


from MPEKUZI

Comments