Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, January Makamba ameziagiza taasisi za umma, kuacha kutumia mkaa kupikia vyakula badala yake zitumie gesi ndani ya mwaka mmoja kuanzia sasa.
Waziri January alitoa kauli hiyo jana kwenye shughuli za upandaji miti zilizofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma alikokwenda kumwakilisha Makamu wa Rais.
Alisema wakati wowote kuanzia sasa ataandika waraka katika taasisi zote kubwa ikiwamo majeshi na vyuo vikuu vyote kwa kuwa mamlaka hiyo anayo kisheria.
“Wengine mtajiuliza nachukua wapi mamlaka hiyo kutoka wapi, natumia sheria ya mazingira kifungu cha 13 ambacho kinanipa mamlaka hayo kwa taasisi yoyote nitakayoona inaharibu mazingira.
“Sheria inanipa nguvu hata kama kuna sheria nyingine hapa inayotoa tafsiri nyingine, inasema sheria hii itakuwa juu yake,” alisema January.
Awali, Naibu Waziri wizara hiyo, Kangi Lugola alisema Serikali haitamsamehe mwekezaji yeyote wa viwanda atakayeharibu, kutiririsha maji au kemikali kwa kisingizio cha uwekezaji wa viwanda.
Lugola alisema kumekuwa na kelele nyingi na visingizio vya Serikali ya viwanda kwa kuanzisha viwanda bila ya kufuata sheria ya mazingira.
Alisema mwekezaji yeyote atakayevunja sheria hiyo hakutakuwa na msamaha badala watamlinda mtu atakayefuata sheria ya viwanda na mazingira.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Godwin Mkanwa alizitaka halmashauri zote kutunga sheria kali kwa ajili ya kulinda hifadhi ya mazingira ikiwamo miti inayopandwa.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment