Baada ya Rais Magufuli, Rais Shein atoa msimamo wake kuhusu muda wa kukaa madarakani

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohammed Shein amesema hayupo tayari kuongeza muda wa uongozi kutoka miaka mitano hadi saba kwani kufanya hivyo ni kukiuka katiba ya Zanzibar.

Dkt Shein amesisitiza kwamba, aliapa kuilinda katiba ya Zanzibar hivyo hawezi kubadilisha muda wa uongozi na hakuna mtu atakayemfanya abadilishe au amvutie yeye kuendelea kukaa madarakani.

Rais Dkt Shein ameyasema hayo jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume visiwani Zanzibar alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baaada ya kurejea kutoka kwenye ziara ya wiki moja katika nchi za Falme za Kiarabu (UAE) alipokua ameambatana na mke wake, Mama Mwanamwema Shein.

“Mimi naheshimu katiba ya Zanzibar, na nina heshimu sheria za Zanzibar. Muda wangu ukifika nitaondoka haraka sana. Hakuna atakayenilazimisha mimi nikae, au atakayenivutia mimi nikae” alisema Rais Dkt Shein.

Aidha, Dkt Shein amesema kuwa, alisikia wawakilishi katika Baraza la Wawakilishi wakizungumza hilo, lakini hawazuiwi kujadili kwani wanafanya hivyo kwa mujibu wa sheria, lakini yeye hayuko tayari kuongeza muda.

“Hilo walizungumza wawakilishi barazani, wana haki ya kuzungumza, kwa mujibu wa taratibu zao na sheria zao na yeyote mwingine anaweza kuzungumza. Mimi nilisikia wakati wananzungumza, Mwakilishi mmoja akasema kwamba kuna baadhi ya nchi duniani zina miaka mitano nyingine saba, sasa kwanini na sisi tusiwe na miaka saba!”

Rais Dkt Shein amesema kuwa, suala la miaka saba labda linaweza kuwepo baada ya yeye kutoka lakini hadhani kama kuna jambo kama hilo.

“Mie sijalisema, sitolisema, na hakuna atayanilazimisha niliseme” alihitimisha Rais Dkt Shein, huku akitilia mkazo kwamba, muda wake ukiisha atamchukua mkewe na kumwambia waondoke.


from MPEKUZI

Comments