Shilingi yaendelea kuwa tulivu dhidi ya dola ya Marekani


Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani imeendelea kuwa tulivu,  ambapo dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,308.87 katika soko la jumla kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Aprili 2022 ikilinganishwa na wastani wa shilingi 2,309.48 katika kipindi cha Julai 2020 hadi Aprili 2021.
Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema hiyo ni sawa na kuongezeka kwa thamani ya shilingi kwa wastani wa asilimia 0.03.

  Ameliambia bunge kuwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani  kuendelea kuwa tulivu kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuwepo kwa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, utulivu wa mfumuko wa bei nchini, mwendelezo wa nakisi ndogo katika urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje, pamoja na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti.

  Kuhusu akiba ya fedha za kigeni amesema, imeendelea kuwa ya kuridhisha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi ambapo hadi kufikia  mwezi Aprili mwaka 2022 akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Marekani bilioni 5.46 ambayo inatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha takribani miezi 4.8.



from MPEKUZI

Comments