Russia: Haitawezekana katu Ukraine kurudi tena kwenye mipaka yake ya zamani


Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Russia Maria Zakharova ameiambia chaneli ya Kiarabu ya Sky News kwamba: "Ukraine tuliyokuwa tukiijua mimi na wewe na iliyokuwepo kwenye mipaka ya awali ya nchi hiyo haipo tena na katu haitakuwepo tena. Hili ni jambo lililo wazi."

Sambamba na kauli hiyo ya Zakharova, rais Leonid Pasechnik wa Jamhuri ya eneo la Luhansk amezungumzia tena mpango wa kuitishwa kura ya maoni kwa ajili ya eneo hilo kujiunga na Russia. Maafisa wa Luhansk wametangaza kuwa, baada ya jamhuri hiyo kurejesha mipaka yake kulingana na namna ilivyoainishwa kwenye katiba yake, suala la kujiunga na Russia "litakuwa ndio kipaumbele cha kwanza".

Mbali na Luhansk, viongozi wa serikali ya kijeshi na kiraia ya eneo la Kherson ambalo tangu katikati ya mwezi Machi limekuwa likishikiliwa na jeshi la Russia wameshasisitiza mara kadhaa kuwa eneo hilo, nalo pia linataka kujiunga na Russia.

Wakati huohuo afisa mmoja mwandamizi wa eneo la Zaporozhye amesema, eneo hilo lina matumaini ya kujiunga na Russia na kuwa sehemu ya eneo la kusini la shirikisho hilo.

Itakumbukwa kuwa, mnamo Februari 21 mwaka huu, Rais Vladimir Putin wa Russia alitoa hotuba ya kuzilaumu nchi za Magharibi kwa kupuuza wasiwasi wa kiusalama wa nchi yake sambamba na kutangaza uamuzi wa kutambua uhuru na kujitawala kwa jamhuri za Donetsk na Luhansk zilizoko katika eneo la Donbas kusini mashariki ya Ukraine. Tarehe 24 ya mwezi huohuo, rais wa Russia alitangaza kuanza kwa alichokiita "operesheni maalumu ya kijeshi" dhidi ya Ukraine; na kwa utaratibu huo, uhusiano wa vuta nikuvute uliopo baina ya Moscow na Kyiv ukabadilika kuwa wa makabiliano ya kijeshi.../
 


from MPEKUZI

Comments