COSOTA yatoa Elimu ya Umuhimu wa Mikataba kwa kazi za Filamu


Na Anitha Jonas – COSOTA, Mbeya  

Wanatasnia wa Filamu wa wasisitizwa kuzingatia suala la mikataba katika kazi zao kuanzia ngazi ya uandishi wa miswada mpaka usambazaji.
 
Msisitizo huo umetolewa leo  Mei 24, 2021 Jijini  Mbeya na Mwanasheria wa Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) Zephania Lyamuya alipokuwa akizungumza na wadau wa tasnia ya filamu Jijini hapo.
 
Akiendelea kuzungumza Bw.Lyamuya alifafanua kuwa suala la mkataba ni jambo la muhimu  katika kulinda hakimiliki na kulinda ubunifu, halikadhalika kutoa ulinzi wa kazi yako hata miaka 50 baada ya mmiliki kufariki.
 
"Katika mikataba hakikisha unaingia mkataba na mmiliki halali wa kazi hiyo, iwe ni mkataba wa kuigiza, Uzalishaji, Uongozaji au Kusambaza na kama ni mkataba wa kuigiza basi ueleze ni uigizaji wa filamu gani kwa jina ili kuepuka matumizi ya kazi hiyo katika kazi ambazo hamjakubaliana,"alisema Bw.Lyamuya.
 
Pamoja na hayo Mwanasheria huyo wa COSOTA  aliwaeleza wadau hao Filamu kuwa wanaweza kupata msaada wa kisheria katika ofisi hiyo na namba ya mawasiliano ni 0738 015 014, pia aliwasisitiza kusajilia kazi zao kwa ajili ya kuzipa ulinzi, ambapo aliwaeleza fomu za usajili zinapatikana kupitia tovuti www.hakimiliki.co.tz.
 
Kwa upande wa Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Dkt.Kiagho Kilonzo aliwaeleza wadau hao wa Filamu kuwa Bodi imeongeza wigo wa biashara ya kazi za Filamu kwa kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi ambapo kwa ndani ya nchi vyombo kama DSTV na Azam Tv wamekuwa wakinunua kazi za Filamu na kutoa ufadhili wa uandaaji wa kazi za filamu.
 
"Tasnia ya Filamu mpaka sasa imetoa ajira kwa takribani elfu ishirini na tano, pia Bodi imepunguza tozo kwa asilimia 90% hivi sasa pia gharama ya kupata kibali sasa hivi ni shilingi elfu hamisi hii imeshuka kutoka shilingi laki tano na ukaguzi wa kazi za Filamu kwa sasa ni shilingi mia tano kwa dakika ambapo awali ilikuwa ni shilingi elfu moja," alisema Dkt.Kilonzo.
 
Aidha, naye Katibu wa Shirikisho la Filamu Tanzania Twiza Mbarouk aliwasihi wadau wa Filamu kujiunga katika vyama na kuwa na umoja na kuacha makundi pia kupunguza maneno ya kulalamika.
   
Vilevile mmoja wa waigizaji wa Filamu Jijini Mbeya Bw.Bahati Tupume aliiomba bodi ya Filamu kufungua ofisi Mbeya na Serikali kudhibiti  filamu za nje zilizotafsiriwa kwani zinadumaza soko la filamu za ndani.




from MPEKUZI

Comments