Hatuendi Kwenye Uchaguzi Kwa Jazba – Majaliwa


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wasichague kiongozi kwa sababu ya jazba au hasira.

Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Oktoba 26, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Nalasi, wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Katani. Mheshimiwa Majaliwa leo amezuru wilaya ya Tunduru akimuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli.

“Hatuendi kwenye chama kwa jazba wala kwa hasira. Hatari ya kipindi hiki unaweza kujikuta unaenda kwenye chama ambacho hakina sera wala hakieleweki. Chama makini kinapaswa kuwa na viongozi wanaoeleweka,” amesema.

Akitoa mfano, Mheshimiwa Majaliwa alisema leo hii kuna chama viongozi wake wamegombana na wala hakina mgombea urais. “Je ukikichagua chama hiki na ukawa na changamoto inakukabili, utaipeleka wapi? Au utampelekea nani? Na ukimchagua diwani au mbunge wa chama hicho, hayo masuala yako atayawakilisha kwa nani?”

“Ninawasihi, unapochagua viongozi, usichague chama kwa sababu maendeleo hayana chama. Chagueni chama ambacho kina mwelekeo na kinajali kutatua shida za watu. Ukienda kupiga kura, chagua diwani, mbunge na Rais anayetoka Chama cha Mapinduzi. Keshokutwa, tumchague Dkt. Magufuli kwa kura nyingi za ndiyo,” amesisitiza.

Mheshimiwa Majaliwa yuko wilayani Tunduru ambako alienda kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Tunduru Kusini, Bw. Adimu Mpakate na wagombea udiwani wa kata nne za jimbo hilo.

Akiwa njiani kuelekea Tunduru, Mheshimiwa Majaliwa alifanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya stendi ya mabasi ya Mangaka, wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.

Akizungumza na wakazi wa Mangaka kwenye mkutano huo, aliwasihi Watanzania wasikubali kuandamana kwa kisingizio cha kutokubali matokeo ya uchaguzi kwa sababu huko ni kuvunja sheria.

“Ninawasihi vijana mjihadhari, msikubali kuandamana kwani mtakuwa mnavunja sheria na mtajikuta mnajiingiza matatizoni. Kuna mtu anakuja hapa na anatulazimisha kuandamana, huyo hafai kuwa Rais wa nchi.”

Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Nanyumbu, Bw. Yahya Muhata na wagombea udiwani wa kata zote za jimbo hilo.


from MPEKUZI

Comments