Biswalo: Hatutavumilia Yoyote Atakayevuruga Amani

SERIKALI imeahidi kumchukulia hatua mtu yoyote atakayeonekana kuvuruga amani ya nchi bila kujali itikadi yake ya kisiasa, dini, wala kabila na kwamba ni wajinu wa kila mwananchi kufuata sheria na taratibu za nchi ili kuepuka vurugu zinazoweza kusababishwa na uvunjifu wa amani.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga wakati wa akifungua Ofisi ya 15 ya Taifa ya Mashtaka nchini, katika mji wa Mafinga wilayani Mufindi, mkoani Iringa huku akitoa angalizo kuwa nchi ambazo hazina amani waathirika wakubwa wamekuwa Watoto, wazee na wanawake hivyo ni jukumu kila mmoja kuwa mlinzi wa amani na usalama wa nchi.

Mkurugenzi huyo wa mashtaka amewaomba Wakuu wa Wilaya zote hapa nchi kuiga mfano wa Wilaya ya Mufindi wa kutoa majengo bure kwa aajili ya kufungua Ofisi ya Mashtaka na kufanya idadi za ofisi hizo kufikia 15 katika wilaya 139 Tanzania nzima jambo ambalo limekuwa likichelewesha usikilizaji wa mashtaka yanapowafikia.

Amesema kuwa ofisi yoyote inayohusika na usalama duniani inajukumu la kulinda amani ya nchi husika pamoja na kuhakikisha watu wake wanafuata sharia na taratibu za nchi hiyo, hivyo wananchi wanaombwa kutoa ushirikiano ili ulinzi, usalama na amani viendelee kutawala nchini.

“Lengo la kufungua ofisi wilayani Mufindi ni kuhakikisha tunaondoa malalamiko, pamoja na kusogeza huduma kwa wananchi na utawala bora ili  kuondoa minong’ono kwa wananchi hasa katika suala la kutendewa haki pindi wanapokuwa na kesi” amesema Biswalo.

Ameongeza kuwa awali huduma hiyo ilikuwa inafuatwa mkoani Mbeya na baadae ofisi ya mkoa ilifunguliwa mkoani Iringa ambapo watu wa Mufindi bado walikuwa wanatumia muda mwingi kuzifuata huduma na sasa ofisi zimefunguliwa wilayani Mufindi.

 “Kumekuwa na minong’ono ya kubambikizwa kesi, jambo hili linapokuja huwa lazima liende katika ofisi za mashtaka sasa ofisi imefunguliwa hapa Mufindi ili kuokoa muda, lakini pia haki itatendeka kwa watu wote na ofisi yetu inafanya kazi kwa kushirikiana na wadau wakubwa ambao ni Mahakama, Jeshi la Polisi, wananchi na Wanahabari hivyo itumieni ofisi hii, ”amesema DPP Mganga


from MPEKUZI

Comments