Taarifa Ya Jeshi La Polisi Mkoa Wa Mbeya

USALAMA KATIKA SIKUKUU YA EID EL FITR.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kuimarisha ulinzi na usalama katika kipindi chote cha kusherehekea sikukuu ya EID EL FITR na hakuna tukio kubwa la uhalifu lililoripotiwa kutokea. Aidha wananchi wamesherehekea kwa Amani na Utulivu huku wakiendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa hatari wa Homa Kali ya Mapafu [COVID 19].

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA SUGU WA MATUKIO YA UVUNJAJI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili [02] 1. KELVIN THOMAS [32] Mkazi wa Mwakibete na 2. SAID KIBIKI [30] Mkazi wa VETA – Ilomba kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya uvunjaji na wizi wa mali mbalimbali.

Watuhumiwa wamekamatwa katika msako uliofanyika kuanzia tarehe 22.05.2020 hadi 26.05.2020 katika maeneo ya Mwakibete, VETA na Pambogo Jijini Mbeya na kufanikiwa kuwakuta na mali mbalimbali za wizi ambazo ni:-

1.     Flat Screen nne [04] za aina mbalimbali.

2.     Radio Sub-Woofer nane [08] za aina mbalimbali

3.     Monitor nne [04] na CPU mbili [02] za Kompyuta.

4.     Amplifier kubwa mbili [02]

5.     Equalizer moja [01]

6.     Hard Disk moja [01]

7.     Spika kumi [10] za aina mbalimbali

8.     Mtungi mmoja wa Jiko la Gesi aina ya Oryx

9.     Keyboard nne [04] za Kompyuta

10. Deck moja aina ya Singsung

11. Stabilizer moja

12. Viatu Jozi nne na Sandles za kiume Jozi moja

13. Vifaa mbalimbali vya kuvunjia.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa mtu yeyote aliyeibiwa vitu vyake kufika Kituo Kikuu cha Polisi Mbeya [Central Police Station] kwa ajili ya utambuzi wa mali hizo. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

KUJERUHI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa nane [08] kutokana na tuhuma za kushiriki kwenye tukio la kujeruhi baada ya kutokea ugomvi kati ya raia wa China wanaomiliki kampuni ya michezo ya kubahatisha “BONANZA” na watu waliokuwa wanacheza mchezo huo.

Ni kwamba mnamo tarehe 25.05.2020 majira ya saa 16:00 jioni huko maeneo ya Soweto, Kata ya Ruanda, Tarafa ya Iyunga, Jiji la Mbeya. Watu wawili ambao ni ABISON HAMISI [36] na GILBERT MWAKANYEMBA [32] Mjasiliamali wote wakazi wa Manga Veta walijeruhiwa kwa kukatwa panga [sime] sehemu mbalimbali za miili yao na raia wa China kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyakazi wao wa kampuni ya michezo ya kubahatisha ya Bonanza.

Chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliozuka kati ya CHEN YEN [43] mfanyabiashara, raia wa China, mkazi wa Veta na ABISON HAMIS @ NDELE baada ya ABISON kutamka neno la kichina lililomuudhi CHEN YEN na kusababisha ugomvi uliopelekea baadhi ya watu kujeruhiwa.

Awali raia huyo wa China alifika eneo hilo kuchukua fedha kwenye mashine ya mchezo wa kubahatisha ya kampuni ya Bonanza akiwa amefuatana na dereva wake GIFT ELIA @ MWAMELO [23] mkazi wa Airport wakiwa na Gari T. 252 DNL Toyota Kluger katika eneo lijulikanalo "Sports Centre" linalomilikiwa na SALUM JUMA. Aidha ABISON HAMIS alifika kucheza Pool akiwa ameongozana na GILBERT MWAKANYEMBA na KENEDY MWAMLIMA na mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la YOHANA.

Kufuatia tukio hilo raia huyo wa China alipiga simu kuomba msaada kwa wenzake ambao ni raia wa China ndipo walifika na kuanza kuwashumbulia ABISON HAMIS @ NDELE na GILBERT MWAKANGEMBA kwa sime maeneo mbalimbali ya miili yao. Aidha ABISON HAMIS @ NDELE na GILBERT MWAKANYEMBA wamelazwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya wakiendelea kupatiwa matibabu.

Pia kufuatia vurugu hizo Gari namba T.252 DNL Toyota Kluger liliharibiwa vibaya kwa kuvunjwa vioo vyote na wananchi wa eneo hilo waliokuwa wakiwashambulia wachina ili kuwaokoa ABISON HAMIS @ NDELE na GILBERT MWAKANYEMBA na upotevu wa mali zikiwemo fedha Tshs 3,000,000, simu ya mkononi aina ya Iphone.

Kutokana na tukio hilo msako mkali umefanyika na watu 8 wamekamatwa ambao ni 1. CHEN YEN [43] mfanyabiashara na mkazi wa Meta, 2. XIAO JING [30] mfanyabiashara na mkazi wa Meta, 3. LIN HAI [30] mfanyabiashara na mkazi wa Meta, 4. LYU JIAN QZING [36] mfanyabiashara na mkazi wa meta, 5. JIANG ZE DONG [39] mfanyabiashara na mkazi wa Meta, 6. GIFT ELIA [23] dereva na mkazi wa Airport, 7. HERMAN ELIAS @ MWALWIBA [20] dereva na mkazi wa Esso na 8. KENED MWAMLIMA [28] dereva, mkazi wa Ituha. Upelelezi wa shauri hili unaendelea.

KUPATIKANA NA BHANGI.

Mnamo tarehe 24.05.2020 majira ya saa 23:30 usiku huko Kitongoji cha Matundasi “A”, Kata ya Matundasi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya.  tulimkamata RICHARD BONIFACE [31] Mkazi wa Matundasi “A” akiwa na bhangi gramu 245. Mtuhumiwa ni muuzaji na mtumiaji wa bhangi.

Imetolewa na:

[ULRICH O. MATEI – SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.


from MPEKUZI

Comments