Wizara Ya Madini Yapongezwa Na Kamati Ya Bunge......Sekta ya Madini yakua kwa asilimia 13.7 ,Ukusanyaji Maduhuli Nusu MwAka Wavuka lengo

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Madini kutokana na mafanikio kadhaa yaliyojitokeza katika Sekta ya Madini ikiwemo Ukuaji wa Sekta ya Madini, Ukusanyaji wa Maduhuli na kueleza kwamba, matunda yanaonekana huku kazi nyingi zikifanywa kwa Mfumo wa Kisasa.
 
Pongezi hizo zinafuatia taarifa mbalimbali za utekelezaji wa  shughuli na miradi iliyotekelezwa na Wizara na Taasisi zake kwa Kipindi cha Nusu Mwaka  kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 ambazo zimewasilishwa kwa kamati hiyo.
 
Kamati ya Bunge imeleza kuwa, Sekta ya Madini imepiga hatua huku ikitoa pongezi kwa Rais Dkt. John Magufuli na kueleza kuwa, sababu za kuitenganisha iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini na kuanzishwa kwa Tume ya Madini zinaonekana.
 
Aidha, Kamati hiyo imetoa ushauri kwa wizara na kuitaka kuendelea kuisimamia sekta ya madini kwa lengo la kuhakikisha kwamba sekta hiyo inazidi kuchangia zaidi katika pato la taifa, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa.
 
Awali, akitoa taarifa kwa Kamati kuhusu hali ya upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa majukumu ya wizara, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini, Augustine Ollal ameieleza Kamati ya Bunge kuwa, kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya Mwaka 2019, Sekta ya Madini ilishika nafasi ya pili kwa kasi ya ukuaji wa asilimia 13.7 ukichangiwa zaidi na ongezeko la uzalishaji wa madini ya dhahabu na makaa ya mawe. 
 
Ameongeza kuwa, hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2019, Wizara kupitia Tume ya Madini ilikusanya maduhuli ya kiasi cha Tsh. 242,531,173,458.83 sawa na asilimia 103 ya lengo la Nusu Mwaka na asilimia 51.5 ya lengo la makusanyo ya mwaka mzima.
 
Akizungumzia mauzo ya madini ya dhahabu kwenye masoko ya madini ameeleza kuwa, kwa kipindi cha Julai hadi Novemba 2019, kiasi cha dhahabu kilichozalishwa katika masoko ya Geita, Chunya, Kahama, Mwanza na Mara kimeongezeka hadi kufikia Kilo 5,546.6 ikilinganishwa na kiasi cha kilo 1,188.4 kipindi cha nyuma kabla ya kuendeshwa kwa kaguzi za kimkakati katika maeneo hayo.
 
‘’Mheshimiwa Mwenyekiti, wizara ilikusudia kuanzisha masoko ya madini katika Mikoa yote nchini, hadi kufikia Mwezi Desemba, 2019 jumla ya masoko 28 na vituo vya ununuzi wa madini 25 yalikuwa yameanzishwa nchini,’’ amesema Ollal.
 
Pia, ameeleza kuwa, baada ya wizara kufanya kaguzi za kimkakati za leseni za biashara ya madini katika maeneo ya Geita, Mara, Mwanza , Chunya, Kahama na  Arusha kumekuwa na ongezeko la leseni  308  kutoka leseni 696 za biashara ya madini kabla ya ukaguzi wa kimkakati kufikia leseni 1004,  huku ongezeko hilo likitajwa  kuchangiwa na kuimarika kwa utendaji wa Tume ya Madini.
 
Vilevile, ameitaja Maabara ya Taasisi ya Jilojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na kueleza kwamba, ilipata ITHIBATI ya Kimataifa ya uchaguzi wa sampuli za dhahabu kwa ya tanuru kutoka shirika la SADCAS na kueleza kwamba, itasaidia sampuli zinazopimwa katika maabara za taasisi hiyo kuweza kuaminika kimataifa na kuruhusu upimaji wa sampuli kutoka nje ya nchi na kupunguza gharama za uchunguzi wa sampuli zetu nje ya nchi.
 
Naye, Waziri wa  Madini Doto Biteko, akizungumza katika kikao hicho, ameileza Kamati hiyo kuwa, Wizara ipo katika mchakato wa kuandaa andiko la kuanzisha Bodi ya Kusimamia Wajiolojia nchini ambayo inalenga katika kudhibiti Wajiolojia wanaotoa taarifa zisizo sahihi kuhusu tafiti za madini nchini. 
 
Aidha, Waziri Biteko ameishukuru Kamati hiyo kwa pongezi na kuendelea kuishauri  na kueleza kuwa, mafanikio hayo yanatokana na kujituma kwa watumishi wa wizara na taasisi zake ikiwemo msukumo mkubwa unaotolewa na Rais Dkt. John Magufuli kwa Sekta hiyo.
 
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwataka wadau wa madini nchini kutekeleza shughuli zao kwa kufuata Sheria na taratibu zilizowekwa na kueleza kuwa, wizara inataka kuona wafanyabiashara wanafanya biashara zao bila kukamatwa kamatwa huku akisema kuwa, wizara itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na shughuli za madini kuwawezesha watanzania zaidi kushiriki na kumiliki uchumi wa madini.
 
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila, ameieleza Kamati hiyo kuwa, katika mkakati wa kuwaendeleza watumishi na kuwajengea uwezo, jumla ya watumishi 12 leo Januari 20, 2020 wanaondoka kuelekea nchini India kwa ajili ya kujifunza  masuala ya Jimolojia ambayo yanahusisha pia masuala ya utambuzi wa madini na uthaminishaji madini na kuongeza kuwa, wizara itaendelea kuangalia nafasi zaidi katika nchi nyingine ikilenga kuwajengea uwezo watumishi kuweza kusimamia sekta hiyo.
 
Mbali na taarifa ya upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa majukumu, taarifa nyingine iliyowasilishwa kwa kamati hiyo ni taarifa kuhusu  hatua zilizofikiwa katika uendelezaji wa Leseni za Mradi wa Liganga na Mchuchuma . Vikao kati ya Wizara na taasisi zake vimeanza leo Januari 20 na vinatarajiwa kuendelea hadi Januari 22, 2020.


from MPEKUZI

Comments