Sekta Ya Afya Nchini Kunufaika Na Msaada Wa Dola Zamarekani Milioni 600 Kutoka Global Fund

Na Ramadhani Kisimba, WFM-Dodoma
Serikali ya Tanzania itanufaika na msaada wa dola za Marekani milioni 600 zitakazotolewa na Taasisi ya Global Fund mwezi Januari mwakani kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na maradhi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria katika  kipindi cha miaka mitatu.

Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Mkuu wa Mfuko huo Barani Afrika Bw. Linden Morrison, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Jijini Dodoma.

Amesema kuwa fedha hizo sawa na takriban shilingi za Tanzania trilioni 1.4 zitatumika kuimarisha afya kwa kupambana na magonjwa ya Ukimwi, Kikufua Kikuu na Malaria ambapo vifaa tiba na vitendanishi mbalimbali vitanunuliwa kupitia msaada huo katika kipindi cha miaka mitatu (2021-2023).

Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka 15 ambacho taasisi yake imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania, Mfuko wake tayari umetoa msaada wa dola za Marekani bilioni 2 kwa ajili ya kusaidia sekta ya afya hususan katika mapambano dhidi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru Taasisi hiyo ya Kimataifa ya Global Fund kwa mchango mkubwa iliyoipatia Tanzania katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo hasa malaria, ugonjwa unaoongoza kusababisha vifo vya watanzania wengi.

Dkt. Mpango aliahidi kwamba fedha hizo zitatumika kikamilifu na kama ilivyokusudiwa ili zilete matokeo chanya kwa kuwafikia walengwa nchini kote.

 ‘‘Nimefurahi kwa sababu nina matumaini kuwa tumepata nguvu ya kupambana na magonjwa haya makubwa, ili Watanzania wawe na afya njema na waweze kujenga uchumi wa nchi yao’’ Alisema Mhe. Mpango.

Aidha Dkt. Mpango alisema katika kikao hicho wamejadili namna ya kuboresha zaidi ushirikiano uliopo kati ya pande hizo mbili ikiwemo kuangalia namna ya kutoa msamaha wa kodi kwenye vifaa yakiwemo magari ya kubebea wagonjwa na dawa zinazoingizwa nchini na Taasisi hiyo kwa ajili ya mradi huo.

“Aidha, Ili kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Taasisi ya Global Fund, nchi itahakikisha inakuwa na ushiriki mpana katika Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko huo ili sauti ya nchi iweze kusikika zaidi” aliongeza Dkt. Mpango

Kuhusu ubadhirifu wa zaidi ya dola za Marekani 400,000 zinazodaiwa kufujwa na baadhi ya Watendaji wa Serikali wanaotekeleza mradi huo hapa nchini, Dkt. Mpango ameuahidi Mfuko huo kwamba Serikali itachunguza na kuwachukulia hatua kali watu wote waliohusika na vitendo hivyo.

Mwisho.


from MPEKUZI

Comments