Waziri Mkuu: Biashara Kati Ya Tanzania Na Urusi Iratibiwe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameutaka ubalozi wa Tanzania nchini Urusi uratibu mipango ya wafanyabiashara wa Urusi wanaokusudia kuja nchini kuwekeza kwa kuwaunganisha na Taasisi na Wizara husika ili waweze kuwekeza mitaji yao kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.

Ametoa agizo hilo jana (Alhamisi, Oktoba 24, 2019) baada ya kugundua uwepo wa wafanyabiashara wengi wa Urusi wanakusudia kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji pamoja na kutafuta wafanyabiashara wa Kitanzania watakaoungana nao katika uwekezaji wanaokusudia kuufanya.

“Tayari miadi imekwishawekwa ya kuwakaribiasha wawekezaji wa Urusi kuja Tanzania kwa ushawishi wa kwangu mwenyewe pamoja na ushawishi wa wafanyabiashara wa Tanzania, hivyo nisingependa wafanyabiashara hao wasumbuliwe au kukatishwa tamaa katika kutimiza nia yao hiyo.” Waziri Mkuu alisisitiza.

Alisema Mkutano baina ya Wakuu wa nchi na Serikali kutoka Mataifa ya Afrika na Urusi uliomalizika jana Oktoba 24, 2019 ulilenga kujenga uhusiano mzuri zaidi katika nyanja mbalimbali hususani za kiuchumi.

Akizungumza baada kumalizika mkutano huo kwenye ukumbi wa Olympic Park wa Sochi nchini Urusi, Waziri Mkuu alisema Urusi imeutumia mkutano huo kueleza bayana maeneo ambayo wako tayari kushirikiana na Afrika katika kuwekeza kwa faida ya pande zote mbili.

Waziri Mkuu aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na uuzaji wa zana za kilimo kama vile matrekta, sekta ya mafuta na gesi pamoja na madini, Ujenzi wa miundombinu hasa reli, masuala ya elimu hasa utoaji wa nafasi za mafunzo nchini humo.

Alisema kwa upande wake Tanzania imejinadi vizuri ikIngozwa na yeye mwenyewe kwani alifanya mazungumzo na viongozi wa makampuni zaidi ya manane ya Urusi ili kuyashawishi yawekeze nchini na yote yalikubali kufika Tanzania mapema iwezekanavyo.

“Viongozi wa makapuni yote niliyopata nafasi ya kuzungumza nao wamesema wako tayari kuja nchini ili waweze kufanya mazungumzo na Serikali pamoja na wafanyabiashara wazalendo ambao wako tayari kuungana na wafanyabiashara hao katika kuwekeza nchini Tanzania.”

Waziri Mkuu alisema viongozi hao walimueleza maeneo ambayo wao wanaamini kuwa wanafanya vizuri na wangependa kupata kibali cha kuwekeza Tanzania baada ya mazungumzo yao na Serikali. Pia walieleza ni kwa namna gani Taifa litanufaika na uwekezaji wao.

Alisema, tayari wafanyabiashara binafsi 18 wa Tanzania walijitokeza kushiriki katika Mkutano huo na walifanya kazi kubwa na nzuri ya kuwahabarisha wenzao wa Urusi kuhusu mazingira mazuri ya kuwekeza yaliyopo nchini hasa baada ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuondoa kero, kanuni na taratibu ziliokuwa zikiyafanya mazingira ya uwekezaji kuwa magumu.

Awali, akizungumza kwenye Mkutano baina ya Wakuu wa nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi, Waziri Mkuu alisema kwa sasa Tanzania ni nchi sahihi kwa uwekezaji kwa wanaotaka kuwekeza barani Afrika kwani imedhamiria kukuza uchumi wake na kufikia wa kati ifikapo 2025 kwa kupitia sekta ya viwanda. Pia ni nchi yenye amani na utulivu.

 “Nchi yetu imejaliwa kuwa na maliasili nyingi ambazo vilele ni malighafi kwa viwanda kama vile mazao ya kilimo, misitu, bahari, maziwa, madini na mbuga za wanyama ambazo ni kivutio cha watalii,” alifafanua Waziri Mkuu.

Leo Oktoba 25, 2019 Mheshimiwa Majaliwa ataondoka nchini Urusi kwenda nchi ya Azerbaijan ambako pia atamwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika Mkutano wa Nchi zisizofungamana na upande wowote. Mkutano huo ni wa siku mbili.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


from MPEKUZI

Comments