Ofisi Ya Makamu Wa Rais Yakutana Na Kamati Ya Kudumu Ya Bunge Ya Viwanda, Biashara Na Mazingira.

Imebainika kuwa Sera ya Usimamizi wa Mazingira (1997) na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na.20 ya mwaka 2004 (Sura ya 191) ndio muundo muhimu wa usimamizi wa mazingira nchini. 
 
Hayo yamesemwa hii leo na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima mara baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango wa pili wa Maendeleo wa miaka mitano katika Sekta ya Mazingira mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira jijini Dodoma.
 
Naibu Waziri Sima amesema katika  kuhusisha masuala ya kuimarisha usimamizi wa rasilimali
Ofisi yake imeandaa Sera, Sheria na Mikakati inayohusiana na uhifadhi wa Rasilimali za  Misitu, vyanzo vya Maji, Ardhi oevu, Wanyamapori, Gesi asilia, Madini na Nishati.
 
Mambo mengine yaliyotekelezwa ni pamoja na kuongoa mifumo ikolojia ya majini iliyoharibika ili kuwepo kwa huduma bora kwa afya ya jamii na ikolojia; kuhifadhi rasilimali za bahari kwa maendeleo endelevu, Miradi na kampeni mbalimbali zimetekelezwa  zikilenga kupunguza uharibifu wa ardhi kwa maendeleo endelevu. 
 
Aidha katika kuimarisha mifumo ya kijamii ya usimamizi wa rasilimali, Naibu Waziri Sima amesema Ofisi yake imeimarisha usimamizi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya nchi kupitia Mradi wa Bonde la Ziwa Nyasa, Mradi wa kurejesha ardhi iliyoharibika, Mradi wa usimamizi endelevu wa ardhi, ambayo yote inasimamiwa na Ofisi yake.
 
Katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa miradi mbalimbali na kukuza teknolojia za nishati jadidifu zinazoweza kurejereshwa (biogas, petroli gesi (LPG), nishati ya jua,pepo na joto la ardhi) pamoja na kusaidia programu za utafiti, kukuza teknolojia mpya, mbegu bora, udhibiti wa wadudu waharibifu, na mbinu bora za kilimo.
 
Wakichangia wasilisho hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Suleiman Saddiq na Kanali Mstaafu Masoud Ali ameishauri Serikali kuwa na Mikakati thabiti ya kuzuia uharibifu wa Mazingira nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ushirikishwaji wa wananchi katika kutunza rasilimali za misitu, ardhi na mazingira yanayowazunguka kwa kushirikiana na wakaguzi wa Mazingira.
 
Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira hii leo imepokea taarifa  ya Ofisi ya Makamu wa Rais –Mazingira kuhusu utekelezaji wa wa Mpango wa miaka mitano wa Maendeleo kwa Sekta ya Mazingira (Mafanikio na changamoto) pamoja na Ripoti ya hali ya mazingira Nchini.


from MPEKUZI

Comments