Mahakama ya Rufaa Yatengua Hukumu na Amri ya Mahakama Kuu kuzuia Wakurugenzi kusimamia Uchaguzi Mkuu

Mahakama ya Rufani Tanzania imetengua uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania iliyobatilisha sheria inayowapa mamlaka Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia Uchaguzi Mkuu.

Kutokana na hatua hiyo, kuanzia sasa Wakurugenzi wapo huru kusimamia uchaguzi.

Uamuzi wa Mahakama ya Rufani, umetolewa na Msajili Elizabeth Mkwizu baada ya Serikali kukata rufaa kupinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu juu ubatilisho wa sheria hiyo.

Katika uamuzi uliosomwa na Msajili wa Mahakama, Mkwizu amesema kuwa miongoni mwa hoja ni kwamba;

Wakurugenzi hawawi wasimamizi wa Uchaguzi moja kwa moja kwa kuteuliwa kwao bali kuna mchakato wa kisheria wanapitia ikiwemo kula kiapo, kutunza siri na kukana uanachama wa Chama walichokuwa nacho kabla ya uteuzi.

Mei 13, 2019 Serikali ilitangaza kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mei 10, 2019 uliotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo ilibatilisha sheria inayowapa mamlaka Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia Uchaguzi Mkuu.

Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Atuganile Ngwala katika kesi ya msingi namba 6 ya mwaka 2018 iliyofunguliwa na mtoto wa marehemu Chacha Wangwe ambaye ni Bob Chacha Wangwe.

Katika kesi hiyo ya Kikatiba, Jaji Ngwala alibatilisha vifungu viwili vya Katiba cha 7 (1) ambapo kinaeleza kuwa ‘Kila Mkurugenzi wa Jiji na Halmashauri wanakuwa wasimamizi wa Uchaguzi Mkuu’

Pia alibatilisha Kifungu cha 7 (3) kinachoeleza kuwa Tume inaweza kumchagua mtu yoyote kuwa msimamizi wa Uchaguzi wakati katiba inasema huwezi kuwa Mwanasiasa na ukawa msimamizi wa uchaguzi bali inatakiwa achaguliwe mtu huru.


from MPEKUZI

Comments