Hatima Ya Wanafunzi Wanaotuhumiwa Kumuuwa Mwanafunzi Mwenzao Yaanza Kuonekana

Na Silvia Mchuruza,Bukoba.
KESI ya mauaji inayowakabili wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Katoro Islamic ya mkoani Kagera wanaotuhumiwa katika mauaji ya mwanafunzi mwenzao, Mudy Muswadiku imeharishwa hadi Novemba 11 mwaka huu kutokana na upelelezi kutokamilika.

Kesi hiyo ya mauaji namba 18/2019 inayosikilizwa na Hakimu Frola Kaijage imetajwa tena leo (jana) katika Mahakama ya Wilaya Bukoba mkoani Kagera ambapo Wakili wa Serikali, Juma Mahona amesema upelelezi wa kesi hiyo unakaribia mwishoni.

Mahona alisema watuhumiwa hao wakiwa gerezani hivi karibuni walitembelewa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) ambapo alisema shauri la watuhumiwa hao liko katika hatua ya mwisho.

“Kwa utaratibu wa makosa ya namna hii RCO anapokamilisha upande wake analeta jarada kwetu na likishafika kwetu tunalipitia ili kuandaa nyaraka kwa ajili ya kupeleka shauri hilo Mahakama Kuu.

Hivyo tumewaambia watuhumiwa wawe wavumilivu, taratibu hizo zitakapokamilika tutawajulisha na kupeleka nyaraka Mahakama Kuu na zikitoka Mahakama Kuu na kurudi Mahakama ya Wilaya hapo ndipo upelelezi utakuwa umekamilika,” Alieleza Mahona.

Kwa upande wa watuhumiwa waliokuwa wakisoma kidato cha nne kufanya mitihani wa Taifa unaotarajia kuanza Novemba 4 mwaka huu, Mahona amesema hawezi kuzungumzia suala hilo maana watuhumiwa waliiomba Mahakama iwaruhusu kufanya mtihani huo.

“Waliiomba Mahakama hivyo wa kulizungumzia suala hilo ni Mahakama yenyewe,” alisema.

Watuhumiwa katika kesi hiyo ya mauaji ya mwanafunzi Mudy aliyekuwa anasoma kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Katoro Islamic ya mkoani Kagera ni wanafunzi Sharifu Amri (19), Fahadi Abdulazizi Kamaga (20), Husama Ramadhan (17), Sharifu Huled (19), Abdalah Juma (19) na Hussein Mussa (20), Majaliwa Abud (35) mwalimu na Badru Issa Tibagililwa (27) mlinzi.

Kesi hiyo imehairishwa hadi Novemba 11 mwaka huu ambapo pia itatajwa tena kwani Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shitaka hilo na watuhumiwa wamerudishwa rumande hadi siku kesi itakapotajwa tena.

Mauji hayo yalitokea Aprili 14 mwaka katika shule ya sekondari ya Katoro Islamic iliyoko katika Halmashauri ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera.


from MPEKUZI

Comments