Waziri Kabudi Akanusha Kuthibitisha Kifo Cha Azory Gwanda

Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema alinukuliwa vibaya kuhusu mwandishi wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) mkoani Pwani, Azory Gwanda.

Profesa Kabudi ametoa ufafanuzi huo leo Alhamisi Julai 11, 2019, akidai alinukuliwa nje ya muktadha wakati akihojiwa jana katika kipindi cha Focus on Africa kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), alipoulizwa swali kuhusu kutoweka kwa Azory tangu Novemba, 2017.

Katika tamko lake kwa vyombo vya habari alilolitoa leo, Profesa Kabudi amesema, “Mpaka sasa hakuna uthibitisho kuwa Azory yuko hai au amefariki. Vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuchunguza tukio hilo na matukio mengine yaliyotokea katika machafuko ya Kibiti, Pwani yaliyosababisha ama watu kadhaa kupoteza maisha au kupotea.”

Azory alitoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana  ambapo mpaka sasa hajapatikana.

Waziri huyo ametoa ufafanuzi kutokana na maelezo aliyoyatoa katika kipindi cha BBC Focus on Africa ambako amekaririwa akisema Azory ni miongoni mwa wananchi waliopotea na kufariki.from MPEKUZI

Comments