Waziri Lugola Asema Mkoa Wa Dar Es Salaam Unaongoza Kwa Biashara Haramu Ya Binadamu Nchini.

Na Felix Mwagara, MOHA, Zanzibar
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza nchini kwa kufanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu huku akitoa onyo kali kwa wanaojihusisha na biashara hiyo.

Akizungumza kabla ya kufungua mafunzo ya siku tano ya Watekelezaji wa sheria ya kuzuia biashara hiyo haramu, katika hoteli ya Ngalawa, mjini Unguja, Zanzibar, Lugola amesema wanaofanya kazi hiyo waiache mara moja maana Serikali itawashughulikia.

“Tatizo hili, linaweza onekana likawa dogo, lakini ukweli ni kwamba sote tunafahamu ni kubwa na limeendelea kukua kila mwaka. Uzoefu wa kiutendaji kutoka Sekretareti hususani kutokana na wahanga wanaookolewa unaonyesha kwamba biashara hii inafanyika sana Mkoa wa Dar es Salaam Tanga, Mwanza, Kigoma, Geita, Dodoma, Singida, Arusha, Manyara, Shinyanga na Tanzania Zanzibar,” alisema Lugola.

Lugola alisema licha ya changamoto hizo, lakini Serikali katika kipindi cha kuanzia Januari mpaka Disemba 2018 imefanikiwa kuwaokoa jumla ya Watanzania 147 waliokuwa wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu. Kati ya wahanga 141walikuwa wakitumikishwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Pia Lugola alisema wahanga 6 walikuwa wakitumikishwa nje ya nchi ambapo watano walikuokolewa kutoka Thailand na mhanga mmoja kutoka Malasia, na Mhanga mmoja aliokolewa hapa nchini alipokuwa akitumikishwa na taratibu za kumrudisha kwao Msumbiji bado zinafanyika.

“Napenda kuwahakikishia Watanzania wote kuwa hatutamuacha salama mtu yeyote, wanaojihusisha na biashara hii waiache mara moja kabla mkono wa sheria haujawafikia,” alisema Lugola.

Aidha, Lugola alisema Serikali ya Tanzania, haijaikataza Watanzania kufanya kazi nje ya nchi, bali imeweka taratibu zenye lengo za kumlinda Mtanzania na madhara yatokanayo na biashara hiyo haramu.

Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara hiyo Haramu kutoka Wizara hiyo, Separatus Fella, alisema zaidi ya washiriki 80 wameshafika katika mkutano wa mafunzo hayo, na matarajio yake makubwa washiriki watapata elimu nzuri kwa ajili ya kupambana na biashara hiyo haramu.

“Mafunzo haya yanatolewa kwa wadau wanaotekeleza sheria ya kuzuia na kupambana na Biashara hiyo, Maafisa Polisi, Uhamiaji, waendesha mashtaka, Mahakimu, Maafisa Ustawi Jamii na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGO’s) yaliyopo Zanzibar,” alisema Lugola.

Fella alifafanua kuwa, mafunzo hayo yanafanyika kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Marekani linalojihusisha na Masuala ya Utafiti (RTI).


from MPEKUZI

Comments