Ufafanuzi Kuhusu Habari Iliyochapishwa Katika Gazeti La Nipashe Kwamba Magereza Yakiri Tatizo Wafungwa Kuingiliana Kinyume Na Maumbile

Katika Gazeti la Nipashe ISSN 0856 NA. 0579874 la tarehe 25 Machi, 2019 ukurasa wake wa kwanza ilichapishwa habari kwamba “MAGEREZA YAKIRI TATIZO WAFUNGWA KUINGILIANA”. 

Aidha, katika ukurasa wa pili (02) wa gazeti hilo, imeelezwa kuwa wafungwa wa kiume katika Gereza la Mkoa wa Shinyanga (Mhumbu), wamedaiwa kufanya ngono kinyume na maumbile, hali iliyoelezwa kuchangia maambukizi ya magonjwa ikiwemo virusi vya UKIMWI.

Jeshi la Magereza linakanusha habari hiyo kwamba wafungwa wa kiume wanaingiliana kimwili katika Gereza Shinyanga na kwamba taarifa hiyo siyo ya kweli. 

Ieleweke kuwa aliyenukuliwa kutoa taarifa hiyo, Ofisa wa Dawati la Jinsia la Magereza Mkoa wa Shinyanga, Victoria Kizito siyo Msemaji wa Jeshi la Magereza na hana mamlaka ya kutoa wala kuthibitisha habari/taarifa kwa niaba ya Jeshi.

Aidha, Sheria za nchi ikiwemo Sheria na kanuni za Jeshi la Magereza zinakataza vitendo vya aina hiyo kwa vile ni kosa la jinai. 

Vitendo hivyo vinadhibitiwa ndani ya magereza kwa kuwaelimisha wafungwa madhara yake na pindi kunapotokea jaribio la mfungwa kujihusisha na vitendo hivyo, Mhusika huchukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa mujibu wa taratibu za Jeshi ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Vyombo vya habari na waandishi mnakumbushwa kuwa taarifa zinazolihusu Jeshi la Magereza hutolewa au kuthibitishwa na Kamishna Jenerali wa Magereza au Msemaji wa Jeshi. Hivyo taarifa zozote zinazotolewa nje ya utaratibu huo zisipokelewe.

Imetolewa na;

P.M. Kasike, 
ndc KAMISHNA JENERALI WA MAGEREZA


from MPEKUZI

Comments