Mgogoro wa Wakulima na Wafugaji wasababisha Mzee mmoja Achomwe Mkuki na kufariki dunia

Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Mzee mmoja aliyetambulika kwa jina la Visu Urembo (80),amefariki dunia baada ya kuchomwa mkuki kwenye sehemu ya ubavuni mwa mwili wake, katika mgogoro wa wakulima na wafugaji, uliotokea Lukenge, tarafa ya Ruvu, Kibaha Vijijini ,mkoani Pwani. 
 
Akithibitisha kutokea kwa tafrani hiyo, kamanda wa polisi mkoani Pwani ACP, Wankyo Nyigesa alisema tukio limetokea majira ya saa 12 alasiri, march 26 mwaka huu. 
 
Alieleza, mzee Urembo kabla ya kufikwa na umauti alikimbizwa kituo cha afya Mlandizi, ambapo baadae alikimbizwa hospital ya Tumbi kwa matibabu zaidi lakini kabla ya kupatiwa matibabu madaktari waligundua kuwa umati umeshamfika. 
 
Hata hivyo, Wankyo alibainisha, wafugaji hao waliingiza mifugo yao (ng’ombe) kwenye bwawa linalotumika katika shughuli za binadamu ikiwemo kunywa, kufulia, kupikia na kadhalika. 
 
“Kwa kuona hivyo ndipo wakulima wakaenda kwa mhemko kuwazuia watoe ng ‘ombe wao lakini wafugaji walianzisha tafrani, ambapo walianza kurusha mikuki ,vitu vyenye ncha kali na kusababisha kifo cha mzee huyo na kujeruhi watu watatu “alifafanua Wankyo. 
 
“Polisi tulifika eneo la tukio alfajir March 27 ,na kutuliza tafrani hiyo na sasa hali ni shwarii”. 
 
Wankyo aliwataja waliojeruhiwa ,kuwa ni pamoja na John Kisukari Urembo (50) ambae ni mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Lukenge. 
 
Wengine ni mtendaji wa kijiji cha Lukenge Maximillian Evarist (34) na Adam Onesha ambae ni mwenyekiti wa kamati ya maji kijijini hapo .
 
Kamanda huyo alitoa wito, jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi ili kuepukana na madhara kama hayo yaliyojitokeza.
Wankyo,alisema kila mtu katika nchi hii ana haki ya kuishi, kutumia ardhi hii, na hakuna mwenye mamlaka juu ya mwenzie ila inabidi kuacha kuingiliana mipaka iliyotengwa kwa ajili ya kundi jingine ili hali kukabiliana na migogoro hasa ya wakulima na wafugaji”alisisitiza Wankyo. 
 
Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama aliyataka makundi hayo yaheshimiane na kujenga upendo badala ya kujiona kundi moja ni zaidi ya kundi jingine.


from MPEKUZI

Comments