Bilioni 50 Zimewanufaisha Wananchi Katika Ujenzi Wa Mji Wa Serikali-ihumwa- Dodoma

Na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imeeleza kuwa takribani Sh. bilioni 50 zimewanufaisha wakandarasi na wananchi wa hali ya chini wakati wa  ujenzi wa ofisi za wizara mbalimbali katika Mji wa Serikali katika eneo la Ihumwa, Jijini Dodoma.

Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, wakati Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, alipotembelea na kukagua ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango katika Mji wa Serikali uliopo eneo la Ihumwa.

Dkt. Mpango alisema kuwa katika eneo la ujenzi kulikuwa na mafundi kutoka kila pembe ya nchi, wafanyabiashara wadogo wa chakula (mama lishe) na wakandarasi ambao wamenufaika na uwekezaji mkubwa wa majengo ya ofisi za Serikali katika eneo hilo la Ihumwa.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la Wizara ya Fedha na Mipango, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, amepongeza maendeleo ya ujenzi wa Ofisi hizo ambao umekamilika kwa asilimia 99.

Waziri Mkuu Majaliwa alimeagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inatengeneza  Bustani nzuri, kusawazisha eneo hilo na kuweka samani katika ofisi hizo ili ziweze kutumika.

Aidha, alimtaka mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kurekebisha kasoro alizozibaini wakati akikagua jengo hilo hususan mlango mkuu wa kuingia ofisi hizo kabla ya kuzinduliwa rasmi na Mhe. Rais hivi Karibuni.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhe. Dkt. Khatib Kazungu, alisema kuwa Wizara imepokea maelekezo ya Waziri Mkuu na kuahidi kuyatekeleza kwa haraka ili watumishi waanze kutumia ofisi hizo.

Mhandisi kutoka NHC, anayesimamia ujenzi huo Bw. Elisante Ulomi ameishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa ushirikiano waliompa katika kufanikisha ujenzi huo ulioanza Desemba 29, 2018 na kuahidi kurekebisha kasoro zilizobainishwa wakati wa ukaguzi huo.


from MPEKUZI

Comments