Waziri wa Nishati Dk. Medad Kalemani Aikabidhi TANESCO Magari 25

Waziri wa Nishati Dk. Medad Kalemani amekabidhi magari 25 yenye thamani Sh.Bilioni 3.1 kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa ajili ya kusimamia miradi wa umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu.
 
Dk.Kalemani alikabidhi magari hayo jsna jijini Dodoma kwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Dk.Tito Mwinuka.
 
Akizungumza kabla ya kukabidhi magari hayo,Waziri Kalemani alisema, magari hayo yatasaidia kurahisisha usafiri katika maeneo ambayo miradi ya Rea awamu ya tatu inatekelezwa.
 
Dk.Kalemani aliitaka, TANESCO kusimamia magari hayo kuhakikisha yanafanya kazi zilizokusudiwa na sio zingine.
 
“Kila gari thamani yake Sh. Milioni 170 na haya ni mpya kabisa sasa nawaomba myatumie kuharakisha miradi ya REA inakamilika na haya magari yasitumike kubeba mikaa na yaende katika vijiji mpaka vitongoji, alisema na kuongeza kuwa
 
...Tanesco sasa hakuna kisingizio magari yapo yasitumike ndivyo sivyo yatumike kwa REA tu, wakandarasi na mafundi michundo ndio watumie, sitaki kusikia anayatumia mtu mwingine,” alisema.
 
Pia Waziri Kalemani alikutana na wadau wanaotekeleza miradi wa REA awamu ya tatu na kujadili jinsi ya kufanikisha mradi huo.
 
Wadau aliokutana nao ni Wakandarasi, Mameneja wa Tanesco Mikoa na Wilaya,Wazalishaji na Wauzaji wa vifaa na Wahandisi kutoka Wizara ya Nishati.
 
Dk.Kalemani aliwataka, Wakandarasi kuhakikisha wanasimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati.
 
“Tumekutana hapa kuoana namna ya kushirikiana hapa kila mdau ana nafasi yake lakini pili kuharakisha kazi ya kusimamia mradi ili ukamilike kwa wakati,” alisema.
 
Mkurugenzi wa TANESCO, Dk.Mwinuka aliahidi kuyasimamia magari hayo kuhakikisha yanafanya kazi iliyokusudiwa. Dk.Mwinuka alisema, magari hayo yatasaidia kufika maeneo ya Vijijini kunakotekelezwa miradi hiyo.
 
“Tutayatunza haya ni magari ya kazi.Kwani katika mikoa 29 tunatekeleza miradi katika mikoa 25,” alisema.
 
Alisema mpango kazi wa Shirika hilo ni kuwafikia wateja wengi kwa muda mchache ili waweze kupata mapato.
 
Akiwasilisha mpango kazi wa REA awamu ya tatu, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Boniface Nyamohanga alisema, mpango kazi ni kuhakikisha kila wiki mkandarasi anaweka umeme katika vijiji vitatu.


from MPEKUZI

Comments