Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Kabudi Afanya Mazungumzo Na Kamishna Wa Haki Za Binadamu Wa Umoja Wa Mataifa

Waziri wa Katiba na Sheria,Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Bi. Michelle Bachelet Jeria Mjini Geneva, Uswisi.

Prof. Kabudi amekutana na Kamishna wakati akihudhuria Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea Mjini Geneva-Uswisi.

Katika mazungumzo yao Kamishna Bachelet alitaka kujua kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu haki za binadamu nchini hususan haki za kina mama na watoto, makundi maalum na kwa jinsi gani Baraza hilo la Mataifa linaweza kuisaidia Tanzania kuendelea kukuza, kudumisha na kulinda haki za binadamu nchini.

Akizungumza katika mazungumzo hayo Prof. Kabudi alisema licha ya Serikali kuendelea na mikakati mbalimbali ya kulinda na kukuza haki za wanawake, imeendelea kutoa fursa kwa wanawake kupata nafasi za uongozi wa juu Serikalini na kwenye taasisi mbalimbali za umma ambazo zinawawezesha kushiriki katika utoaji wa maamuzi yenye manufaa kwa nchi.

Prof. Kabudi alisema Tanzania inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari na uwepo wa vyama vya siasa na demokrasia nchini na kuongeza kuwa mwaka huu inatarajia kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utafuatiwa na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2020.

Prof. Kabudi alimhakikishia Kamishna Bachelet kuwa Tanzania itaendelea na jitihada za kukuza, kuheshimu na kulinda haki za binadamu nchini pamoja na kutekeleza wajibu wake na ahadi zake mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Aidha Prof. Kabudi alielezea jitihada zinazofanwa na Serikali kwenye maeneo ya elimu, afya, mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya pamoja na malengo ya kuleta maendeleo nchini.

Prof. Kabudi alisema Serikali imeboresha mfumo wa ukusanyaji kodi na hivyo kuiwezesha Serikali kutoa huduma za kijamii kwa wananchi wake bila ubaguzi.

Mhe. Kabudi alimshukuru Kamishna Bachelet kwa ushirikiano uliopo kati ya Ofisi yake na Wizara ya Katiba na Sheria na Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania Mjini Geneva-Uswisi na kwamba Serikali kwa ujumla itaendelea na mazungumzo kuhusu maeneo ambayo wataweza kushirikiana.

Ofisi ya Kamishna ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu iliundwa mwaka 1993 ili kusimamia ukuzaji na ulinzi wa haki za binadamu duniani. Ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu pamoja na mambo mengine inazisaidia Serikali za nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa kutoa mafunzo na utaalamu kwenye maeneo ya upatikanaji wa haki, mabadiliko ya sheria na masuala ya uchaguzi. Vile vile inazisadia Serikali za Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutekeleza wajibu walionao kimataifa wa kulinda, kuheshimu na kukuza haki za binadamu.


from MPEKUZI

Comments