Watu 7 Wafikishwa Mahakamani Mauaji ya Watoto Njombe

Na Amiri kilagalila Njombe
Watu saba wamefikishwa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe  kwa tuhuma za mauaji ya watoto mkoani Njombe yanayohusishwa na imani za kishirikina.

Mmoja wa watuhumiwa hao ni David Kasila ambaye alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe februari 18 mwaka huu akituhumiwa kuwaua watoto watatu ambao ni Oliver Ng’ahala(5),Goodluck Mfugale(5)Meshack Myonga(4) wote ni wakazi wa wilaya ya Njombe.

Watuhumiwa wengine ni Mariano Malekela,Edwini Malekela,kalistus Costa wakazi kijiji cha Matembwe tarafa ya Lupembe walifikishwa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe mnamo februari 19 mwaka huu kwa tuhuma za kumuua mtoto wao Rachel Malekela(7) februari moja mwaka huu ambapo mwili wake ulikutwa mita 50 kutoka nyumbani kwao akiwa amechinjwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana kamanda wa polisi Mkoa wa Njombe Renata Mzinga,alisema kati ya watuhumiwa 49 waliokuwa wakishikiliwa na jeshi la polisi baada upelelezi watuhumiwa saba pekee ndio walikutwa na hatia na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma hizo.

‘’Hata hivyo oparesheni zetu ziliendelea hadi tulipofika mikoa jirani ya Mbeya,Iringa na hata Songea ambako tuliweza kuwapata watu mbalimbali pamoja na msako wetu tuliendelea kuwakamata waganga wa jadi na hasa wale wapiga ramli chonganishi ambao waliweza kuchochea chuki katika mkoa wetu’’alisema Renata.

Alisema jeshi la Polisi  limewafikisha mahakamani watu saba,watatu kwa tukio la mauaji ya watoto watatu kijiji cha Ikando,mtuhumiwa mmoja kwa mauaji ya watoto watatu mjini Njombe,na watuhumiwa watatu kwa mauaji ya mtoto mmoja kijiji cha Matembwe.

Alisema kutokakana na oparesheni iliyofanyika wanaendelea kuwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za mtu yoyote atakaebainika na kuwa na dalili zozote za kujihusisha kwenye mauaji hayo.

‘’Tunaomba wananchi waendelee kutuletea taarifa ambazo ni za kweli. taarifa ambazo zitaweza kutusaidia sio taarifa za fitina au za kukomoa watu wakidai kuwa wanajihusisha na matukio haya kwa mfano wananchi wanaotuletea taarifa za maandishi wakieleza kuwa kuna matumizi ya gari namba zimehifadhiwa,kuna watu walioshuhudia majina yamehifadhiwa kuna gereji zinazotumika kuficha waalifu jina la gereji limehifadhiwa hapo itatuletea ugumu  sisi polisi kukamilisha upelelezi wetu’’alisema.

‘’Tunaomba taarifa za kueleweka ili kuweza kukomesha mauaji haya moja kwa moja sio taarifa ambazo zinaeleza majina yamehifadhiwa,sisi tunazichukulia kama taarifa za majungu ambazo hazina utafiti wowote na haziwezi kutuletea mafanikio.pia wananchi waendelee kutuletea taarifa za waganga wa jadi hasa wale wapiga ramli chonganishi ili tuwakamate na kuwafikisha mahakamani’’alisema Renata.

Pia Kamanda huyo amewataka wazazi na walimu kuendelea kushirikiana kuwalea watoto sambamba na kuwaasa wananchi waache kuamini imani za kishirikina na badala yake wafanye shughuli halali ili waweze kuhakikisha jamii inakuwa salama.

Kamanda Mzinga alisema wananchi wazingatie taratibu za kisheria kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi na wafuate taratibu za mirathi ili kuepuka kufanya mgawanyo wa mali kwa kutumia ubabe na visasi.

Aidha jeshi la polisi  mkoa wa Njombe linaendelea na upelelezi juu ya mtoto Gaudes Kihombo(7) mkazi wa kijiji cha Ikando kata ya Kichiwa aliyepotea tangu Januari sita ambaye hadi sasa hajapatikana.

Mpaka sasa watuhumiwa saba wamefikishwa mahakama ya hakimu mkoa wa Njombe kwa matukio ya mauaji ya watoto nane wakiwemo wa familia moja.


from MPEKUZI

Comments