Wabunge wawili wa Chadema, Peter Lijualikali na Susan Kiwanga Wafikishwa Mahakamani

Wabunge wawili wa Chadema, Peter Lijualikali (Kilombero) na Susan Kiwanga wa Mlimba na wenzao saba wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro baada ya kukamatwa na polisi.

Kwa mujibu wa  Kaimu Katibu wa Vijana Chadema mkoa wa Morogoro, Jackson Malisa, Wabunge hao walikamatwa Jumatano iliyopita ya Februari 20, 2019 wakiwa Kijiji cha Sofi wilaya ya Malinyi na kukaa rumande hadi leo Jumatatu Februari 25, 2019.

Bado haijafahamika wabunge hao na wenzao wana tuhuma gani, lakini wiki iliyopita Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa alisema jeshi hilo  lilikuwa linawasaka wabunge hao pamoja na wanachama 11 wa Chadema walioachiwa huru na mahakama mkoani humo Januari  2019.

Waliachiwa huru kupitia kifungu cha Sheria namba 225 cha mwenendo wa makosa ya jinai baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yanawakabili, ikiwa ni pamoja na kuchoma moto ofisi ya Sekondari ya kijiji cha Sofi Wilaya ya Malinyi.

Mutafungwa  alisema kuwa  jeshi la Polisi hivi sasa wamejipanga kwa kuwa na ushahidi na vielelezo vya kutosha vya kuwatia hatiani watuhumiwa hao waliokuwa  wameachiwa huru na Mahakama.


from MPEKUZI

Comments