Urusi yaituhumu Marekani kutaka kuiingilia kijeshi Venezuela

Urusi imeelezea wasiwasi wake kwamba Marekani inajiandaa kuiingilia Venezuela kijeshi, kufuatia hatua kadhaa za kijeshi zinazofanywa na taifa hilo katika ukanda huo, ambazo Urusi inadai kwamba ni maandalizi ya kumuondoa rais Nicolas Maduro madarakani. 

Marekani inamuunga mkono, kiongozi wa upinzani Juan Guaido, aliyejitangaza kuwa rais wa mpito nchini humo.

Katibu wa baraza la usalama la Urusi Nikolai Patrushev, amenukuliwa na vyombo vya habari nchini humo akisema kuhamishwa kwa vikosi vya operesheni maalumu vya Marekani nchini Puerto Rico, kuwasili kwa vikosi Colombia na mambo mengine yanaashiria kwamba wizara ya ulinzi ya Marekani inapeleka vikosi vyake kwenye ukanda huo ili kuvitumia kwenye operesheni ya kumuondoa Maduro.

Amesema, Urusi ilikubaliana na mapendekezo kutoka Marekani kuhusu mashauriano ya mzozo wa Venezuela, nchi ambayo ni mshirika wa karibu wa Moscow, lakini Marekani mara kadhaa imeliahirisha pendekezo hilo.

Mapema, makamu wa rais wa Marekani Mike Pence pamoja na kiongozi wa upinzani, Juan Guaido walikubaliana kuhusu mkakati wa kuimarisha vikwazo dhidi ya watu wanaomzunguka rais Nicolas Maduro, kufuatia mkutano wake na washirika wa kikanda nchini Colombia mnamo siku ya Jumatatu.
 
Makamu wa rais wa Marekani, Mike Pence ametangaza vikwazo zaidi dhidi ya Venezuela na dola milioni 56 za msaada kwa taifa hilo jirani, linalokimbiwa na idadi kubwa ya raia wake  kutokana na hali mbaya ya kiuchumi. 

Amesema wanataraji kuwepo kwa mabadilishano ya mamlaka kwa amani, lakini rais Donald Trump wa Marekani ameliweka hilo wazi, akisema mapendekezo yote yako mezani.

Maduro, alijibu hatua hiyo kwenye mahojiano yaliyofanyika siku hiyohiyo, akisema mkutano wa kikanda ulilenga kuandaa serikali yenye usawa na kuituhumu Marekani kwa kutaka kufanya lolote, hata kuingia vitani  ili kuweza kupata mafuta yake.

-DW


from MPEKUZI

Comments