Serikali Yakarabati Shule Zake Kongwe Za Serikali Ili Kuboresha Elimu

Na Benny Mwaipaja, WFM, Kibaha
Serikali imetoa zaidi ya  sh. bilioni 42 kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya Sekondari 42 kati ya shule 88 kongwe zilizopo nchini kote ikiwemo shule ya Sekondari Ruvu iliyoko Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.

Akizungumza mara baada ya kukagua ukarabati wa shule hiyo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa shule zote Kongwe ambazo zinahistoria kubwa ya kutoa viongozi wengi na wataalam mbalimbali nchini, zinakuwa na hadhi na kuwa kimbilio la wananchi.

Ametoa wito kwa uongozi wa shule hiyo ya Sekondari ya Wasichana Ruvu, kuhakikisha kuwa elimu bora inatolewa kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ili thamani ya uwekezaji mkubwa wa Serikali unaofikia zaidi ya shilingi bilioni 990 uweze kuonekana

"Dhamira yetu ni kuona watoto wetu wanasoma kwenye mazingira sahihi na ufaulu wao unaongeeaka kwa sababu tunawaandaa wataalam wa kesho wa Taifa letu" Aliosisitiza Dkt. Kijaji

Alisema amejionea ukarabati uliofanyika shuleni hapo ambapo pamoja na shilingi milioni 992 kutumika katika ukarabati huo, bado nyumba 6 za walimu hazijakarabatiwa pamoja na kutonunuliwa kwa samani za shule vikiwemo vitanda na kuahidi kuifanyia kazi changamoto hiyo wakati wa huu wa mchakato wa bajeti mpya

Kwa upande wao, Mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Juma na Mkuu wa Shule hiyo, Juliana Chimazi, wameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha shule hiyo na kuomba wapatiwe fedha kwa ajili ya kununulia samani hasa vitanda kwa ajili ya wanafunzi ili kwenda sambamba na uboreshaji mkubwa wa majengo uliofanyika shuleni hapo.

Mkuu wa shule hiyo Mwl. Juliana Chimazi alimweleza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji kwamba shule hiyo inahitaji vitanda vipya kwa kuwa vilivyopo vimedumu zaidi ya miaka 50 pamoja na kuomba fedha kwa ajili ya kukamilisha ukarabati wa nyumba sita za walimu.

Miongoni mwa miundombinu iliyoboreshwa katika shule hiyo ya Sekondari ya washichana Ruvu ni pamoja na mifumo ya maji taka, madarasa, vyoo, mabweni, nyumba za walimu na Ofisi.

Naibu Waziri Dkt. Kijaji anaendelea na ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali iliyopewa fedha na Serikali ikiwemo ya kimkakati inayolenga kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kujitekemea kwa mapato.

Mwisho


from MPEKUZI

Comments