Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Akabidhi Kompyuta 25 Ludewa Kuongeza Kiwango Cha Ufaulu Shule Za Sekondari

Na Amiri Kilagalila
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amegawa kompyuta 25 kwa shule za sekondari za Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe zenye thamani ya shilingi milioni 48 kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kujifunzia na waalimu kufundishia, kuongeza uelewa na kupata maarifa kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuunganisha kompyuta hizo na mtandao wa intaneti ili kuwawezesha wanafunzi wa Wilaya hiyo kuongeza kiwango cha ufaulu

Nditiye amekabidhi kompyuta hizo kwa Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Ludewa ili ziweze kutumika kwenye shule mbali mbali zilizopo Wilayani humo

“Nimeleta kompyuta 25 ili zigawiwe kwenye shule mbalimbali ili watoto wajifunze kutumia TEHAMA pamoja na waalimu waliopewa mafunzo ya TEHAMA na taasisi yetu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)”, amesema Nditiye. 

Kompyuta hizo zimetolewa na UCSAF ambayo inahusika na ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara

Nditiye ameongeza kuwa Wilaya ya Ludewa inafahamika katika kipindi cha miaka ya nyuma kwa kuwa moja ya Wilaya saba nchini ambapo wanafunzi wake wana kipaji cha akili ukilinganisha na Wilaya nyingine zilizopo nchini ambapo ameona ni vema kuwapatia wanafunzi wa shule za Wilaya hiyo kompyuta hizo ili waweze kuongeza ufaulu, kujenga uelewa na kupata maarifa ili waweze kuwa wanafunzi vinara kama iliivyokuwa imezoeleka katika kipindi cha miaka ya nyuma. Pia, amesema kuwa Tanzania inaongoza katika matumizi ya TEHAMA katika Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mara baada ya kupokea kompyuta hizo kwa niaba ya wananchi, Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa alimuomba Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Andrea Tsere kuwa, kuwe na kituo kimoja cha kutunga mitihani Ludewa ili waalimu watunge mtihani wa aina moja na waweze kumaliza kufundisha masomo ya kiada na ziada kama walivyopanga kwa muhula husika wa masomo ili waweze kuwapima wanafunzi wote kwa pamoja

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Andrea Tsere alimueleza Nditiye kuwa wataweka intaneti kwenye kompyuta hizo ili waalimu na wanafunzi waweze kupata notisi. Pia, amesema kuwa kompyuta hizo zitatumika kuinua kiwango cha elimu na zimefika muda muafaka

“Mmetusaidia sana, umeingia kwenye akili yangu ya kuinua kiwango cha elimu Ludewa,” amesisitiza Tsere wakati akimshukuru Nditiye kwa kuzipatia shule za Wilaya yake kompyuta 25. Tsere amewataka waalimu wakuu wa shule kuzitunza kompyuta hizo na kuzifanyia matengenezo pindi inapohitajika badala ya kuacha ziharibike na pasipo kuzipanga vizuri kwa sababu ni vifaa vya Serikali badala yake wanapanga lini wavichukue badala ya kuzitunza vizuri ili zisaidie wanafunzi wengi na kwa muda mrefu. Aidha, amesisitiza kwa waalimu hao kuwa kompyuta zikipotea na wao wapotee

Katika hatua nyingine, Nditiye amewaeleza wananchi hao kuwa, Wizara yake ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia UCSAF imetoa ruzuku kwa kampuni ya simu ya Halotel na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ili wajenge minara 11 kwenye maeneo ya mwambao kwa wananchi waishio Wilayani Ludewa kwa kuwa hawana mawasiliano.

“Tunahitaji Ludewa iwasiliane na dunia,” amesisitiza Nditye. Amefafanua kuwa minara tisa imejengwa na kampuni ya Halotel na miwili ni ya TTCL

Vile vile, ameongeza kuwa, ujenzi wa meli ya abiria waishio Ludewa kwa ajili ya usafiri wa Ziwa Nyasa umekamilika ambapo kwa sasa meli hiyo inafanyiwa majaribio kabla ya kuanza safari zake na Serikali inakamilisha ujenzi wa gati za kushusha na kupakia abiria kwenye mwambao wa ziwa hilo kwenye maeneo ya Manda, Lupingu, Nsele, Yiga na Nkanda ambapo meli hiyo inatarajiwa kuanza safari zake za kutoka Ludewa, Njombe hadi Kyela, Mbeya mwezi Aprili mwaka huu

“Tunataka Lupingu hadi Matema watu wapite kwa lami,” amefafanua Nditiye. Ameyasema hayo wakati akiongea na wananchi wa Ludewa mjini na kuwaeleza kuwa  azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa barabara ya Lusitu – Mawengi yenye urefu wa kilomita 50 inajengwa kwa kiwango cha zege kwa gharama ya shilingi bilioni 159 ambapo tayari mkandarasi wa kutoka nchi ya Korea yupo na anaendelea na ujenzi wa barabara hiyo ili iweze kupitisha madini ya Mchuchuma na Liganga

Ngalawa amewaeleza wananchi kuwa anamshukuru Nditiye kwa kuwa alifanya ziara kutoka Lupingu hadi Manda mwaka jana mwezi wa tatu akiwa na miezi minne tu tangu alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri na kushuhudia ukosefu wa mawasiliano kwa wananchi waishio mwambao na sasa minara 11 imejengwa ambapo tayari minara mitatu ya Nkanda, Mawengi na Mahong’olo imewashawa na meli ya abiria pia itaanza safari zake

Tsere alimshukuru Ngalawa kwa kumleta Nditiye ambapo alisafiri na boti siku nzima Ziwani mwaka jana mwezi wa Machi na kushuhudia ukosefu wa mawasiliano kwa kuwa tangu dunia iumbwe wananchi wa mwambao hawajawahi kupata mawasiliano na sasa wanawasiliana.


from MPEKUZI

Comments