Naibu Waziri Kanyasu Atoa Mbinu Ya Kuzibana Halmashauri Kupanda Miti Milioni 1.5

NA LUSUNGU HELELA-WMU
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameshauri itungwe sheria ya  kuhakikisha kila  Halmashauri nchini inapanda  miti milioni 1.5 kila mwaka ili kukabiliana na tatizo la  uharibifu wa mazingira nchini
 
Hatua hiyo inakuja baada ya agizo la Makamu wa Rais, Mhe.Samia Suluhu Hassan  alilolitoa wakati alipokuwa akizindua kampeni ya kuifanya Dodoma kuwa ya kijani mwezi  Disemba 2018  kuwa kila Halmashauri ihakikishe inapanda miti milioni 1.5 kila mwaka.
 
Amesema hata hivyo tangu agizo hilo lilipotolewa hakuna Halmashauri hata moja iliyoweza kulitekeleza agizo hilo badala yake Halmashauri zilizo nyingi zimekuwa zikitaja takwimu za uongo.

Akizungumza mbele ya Makamu wa Rais, Mhe.Samia Suluhu Hassan kwenye  kongamano la kulinda Mazingira lililofanyika kitaifa mkoani Tabora, Mhe.Kanyasu ameshauri itungwe sheria itakayowabana Wakurugenzi kutekeleza agizo hilo.
 
Amesema endapo agizo hilo likapitishwa na bunge na baadaye kuwa sheria Wakurugenzi watalazimika kupanda idadi hiyo ya miti badala ya ilivyo sasa kila Mkurugenzi kutekeleza agizo hilo kama hiyari.
 
Ameeleza kuwa Halmashauri zilizo nyingi zimekuwa zikitaja takwimu kubwa za miti iliyopandwa lakini anapokwenda kwa ajili ya kuiona  wmiti hiyo imekuwa haionekani na huku  wengine wamekuwa wakiibuka na visingizio kwa vile hakuna idadi hiyo ya miti waliyoipanda.
 
Amesema idadi ya miti ambayo imekuwa ikitajwa na Halmashauri kupandwa imekuwa ya vitabuni isiyo na uhalisia wa aina  yoyote.
 
Ameongeza kuwa hata zile Halmashauri ambazo zimekuwa zikijaribu kupanda zimekuwa hazifikishi idadi hiyo hata zikishapanda zimekuwa hazijishughulishi na kufuatia maendeleo ya miti hiyo.
 
Amesema hali hiyo imepelekea miti iliyo mingi kufa kwa kukosa uangalizi huku mengine kuliwa na mifugo wakati  Halmashauri hizo zimekuwa zikibaki na takwimu zile zile za miti waliyoipanda.
 
Akizungumza Makamu wa Rais, Mhe.Samia Suluhu Hassani amesema agizo lake lililenga  kila Halmashauri ipande miti milioni 1.5 ikiwa ni lazima na sio hiyari kama Halmashauri zinavyotekeleza.
 
Hata hivyo, Mhe. Samia ameeleza kuwa katika agizo hilo lilikuwa wazi liikitaka kila Halmashauri  ihakikishe inapanda  miti ya aina yoyote ile akitolea mfano mizabibu, miti ya matunda ili mradi tu uwe mti bila kujali miti ya aina gani.
 
Ameongeza kuwa kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea nchini, Ofisi yake itahakikisha taratibu zinafuatwa za kulifanya agizo hilo liwe sheria.


from MPEKUZI

Comments