Mwili Uliokaa Mochwari Miezi 8 Wazikwa Mbeya

Mwili wa Kijana Frank Kapange (22) aliyefariki zaidi ya miezi nane  na siku 26 na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, umechukuliwa na ndugu  kwenda kuzikwa katika kijiji cha Syukula katika Wilaya ya Rungwe  mkoani Mbeya  baada Mahakama kuamuru mwili huo kuzikwa.
 
Akizungumza  hospitalini hapo, Msemaji wa Familia, Julius Kapange amesema kupitia mahakama mbalimbali mkoani Mbeya  waliomba mwili ufanyiwe uchunguzi ili kujua sababu za kifo cha kijana wao  ambaye anadaiwa kufariki  kwenye mazingira ya kutatanisha lakini  waliamuriwa kuuzika mwili huo ndani ya wiki moja vinginevyo Halmashauri ya Jiji ingezika.

Shangazi wa marehemu Sophia Kapange amesema hawakususia mwili bali walitaka kujua sababu za kifo cha mtoto wao ndiyo maana walikuwa wakifuatilia mahakamani ili haki itendeke lakini imekua tofauti na matarajio yao huku  Mama mzazi wa marehemu akidai  kifo cha mwanae kimekuwa pigo kwake kwani  alikuwa akiendesha familia kwa kufanya biashara ndogo ndogo katika Soko la Sido.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Godlove Mbwanji amesema wameamua kusamehe gharama zote za  kutunzia mwili wa marehemu  ili fedha ambazo waliziandaa zikatumike kwenye msiba.

Frank alifariki Juni 4, 2018 huku kifo chake kikigubikwa na utata kutokana na mazingira yake baada ya ndugu kudai kijana wao ambaye alikuwa ni mfanyabiashara wa nguo za mitumba soko la Sido jijini Mbeya alifariki kwa kipigo akiwa mikononi mwa polisi hivyo ndugu waligoma kumchukua na kwenda kumzika.


from MPEKUZI

Comments