Mkurugenzi UDART na wenzake wawili kwenda kuhojiwa TAKUKURU

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumhoji Mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (UDART) Robert Kisena (46) na wenzake wawili.

Kisena ambaye jana hakufika Mahakamani kwa sababu anaumwa na wenzake watatu ambao ni Kulwa Kisena(33) na Charles Newe(47) wanakabiliwa na mashtaka 19 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kuusababishia Mradi wa UDART hasara ya zaidi ya Bilioni. 2.41.

Maombi hayo yaliwasilishwa Mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Simon alidai kuwa wanawaomba washtakiwa hao kwenda kuhojiwa kwa siku moja TAKUKURU kisha kurudishwa na kubainisha kuwa mshtakiwa wa kwanza Kisena ameshindwa kufika mahakamani hapo kwa sababu ni mgonjwa.

Hata hivyo mahakama hiyo imeridhia washtakiwa hao kuhojiwa na kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 11, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa hao na mwenzao mmoja ambaye ni raia wa China, Cheni Shi (32) walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 11, 2019 na kusomewa mashtaka 19 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kuusababisha mradi huo hasara ya zaidi ya Bilioni. 2.41.

Katika mashtaka hayo, lipo shtaka moja la kuongoza uhalifu, lingine moja la kujenga kituo cha mafuta bila kibali, la kuuza mafuta sehemu zisizoruhusiwa pamoja na shtaka la wizi wakiwa Wakurugenzi.

Pia wanakabiliwa na mashtaka manne ya utakatishaji fedha, ya kughushi manne, kutoa nyaraka za uongo manne, mashtaka mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na shtaka moja la kuisababishia mradi huo hasara.


from MPEKUZI

Comments