Bima ya Taifa (NHIF) Watakiwa kutochelewesha Kadi za Wanachama

Na WAMJW – MTWARA
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameuagiza uongozi wa  wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutatua changamoto ya uchelewaji wa vitambulisho vya bima ya afya kwa wananchi.

Ameyasema hayo mapema leo wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utendaji kazi wa mfuko huo Mkoa wa Mtwara, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya Mkoani hapo.

DKt. Ndugulile amesema kuwa NHIF ni lazima ihakikishe inawahudumia vizuri wananchi wanaokuja kujiunga katika mfuko huo, ikiwemo kuhakikisha ndani ya wiki mbili baada ya kujaza fomu, wateja wapate kadi zao.

“Tuendelee kuwahudumia vizuri, na kuhakikisha kwamba, ndani ya wiki mbili baada ya kujaza fomu na kukamilisha taratibu, waweze kupata kadi zao” alisema DKt. Ndugulile

Pia, Dkt. Ndugulile amesema Serikali imeridhishwa kwa kiasi kikubwa na mwitikio mzuri wa wananchi kujiunga na Bima ya Ushirika jambo litalowasaidia kupata huduma za afya katika vituo takribani 6,000 nchi nzima.

Aidha, Dkt. Ndugulile ameagiza NHIF kuweka utaratibu wa kuwafuata na kuwapatia kadi za bima wateja waliojiandikisha ili kuweka hamasa kwa wananchi wengine kujiunga na bima ya afya na kuwapunguzia usumbufu.

Mbali ya hayo DKt. Ndugulile ametoa onyo kwa watoa huduma za afya wanaofanya udanganyifu, na kuwataka watoe huduma kwa kufata sheria, na kwa mujibu wa miongozo ya Wizara ya Afya,

DKt. Ndugulile aliendelea kusema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za maboresho ya sheria ambazo zitatoa adhabu kali kwa yeyote atakayehusika na udanganyifu wowote utaopelekea hasara kwa Serikali.

Kwa upande mwingine DKt. Ndugulile amewaagiza watoa huduma za afya kuhakikisha wanawasilisha madai yao kwa NHIF kwa wakati, huku akisisitiza kuwa NHIF nayo inapaswa kulipa madeni kwa wakati.

“Haipendezi wananchi wanahudumiwa katika vituo vyetu vya kutolea huduma za Afya, na madai yanakaa zaidi ya miezi miwili au mitatu, kwahiyo niombe watoa huduma waharakishe madai yao, ili waweze kulipwa kwa wakati” alisema DKt. Ndugulile.

Nae Mkulima wa Korosho kutoka Halmashauri ya Nanyamba kijiji cha Nyundo, amewataka wakulima kupitia vyama vya Ushirika wajiunge na Bima ya Afya ili kuepuka gharama kubwa za matibabu na ugonjwa hauchagui muda wa kuja.

“Nimehamasika kujiunga na bima ya afya baada ya kuelewa kwamba ukulima una muda wa kupata pesa na una muda wa kukosa, alafu homa haichagui muda,” alisema Bw. Said Akili.

Aidha Bw. Said Akili ameiomba Serikali kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya hasa kwa Wateja wanaotumia kadi za Bima ya Afya, jambo litalo wahamasisha wakulima wengi zaidi kujiunga na mfuko huo.


from MPEKUZI

Comments