Waziri wa Kilimo Ashuhudia Hafla Ya Utiaji Saini Mikataba Ya Ubanguaji Korosho Tani 7500

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) jana Tarehe 10 Januari 2019 ameshuhudia hafla ya utiaji saini mikataba ya ubanguaji korosho kati ya Bodi ya nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania na wenye viwanda vya ndani.

Mkurugenzi wa Bodi ya nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania Dkt Hussein Mansoor ndiye ametia saini kwa niaba ya serikali na Kampuni nne zimesaini mikataba ya awali kuanza kazi hiyo ambazo ni kampuni ya Hawte Investment Co. Ltd, Micronix Mtwara, Korosho Afrika, na Micronix-Newala.

Kampuni hizo zimeingia mikataba ya Jumla ya Tani 7500 ambapo kampuni ya Hawte Investment Co. Ltd yenye uwezo wa kubangua Tani 2000 kwa mwaka imesaini mkataba wa Tani 1500.

Kampuni ya Micronix ya mjini Mtwara yenye uwezo wa kubangua Tani 2400 kwa mwaka imeingia mkataba wa Tani 1200. Kampuni ya Korosho Afrika ya Mjini Tunduru Mkaoni Ruvuma yenye uwezo wa kubangua Tani 5000 kwa mwaka imeingia mkataba wa kubangua Tani 2400 ilihali Kampuni ya Micronix ya Wilayani Newala yenye uwezo wa kubangu Tani 5000 kwa mwaka imeingia mkataba wa kubangua Tani 2400.

Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa serikali imepitia vifungu vyote vya kisheria kabla ya kuanza kuingia makubaliano na kampuni hizo kwa ajili ya ubanguaji wa Korosho.

Alisema kuwa zoezi la ubanguaji tayari lilikuwa limeanza kupitia Shirika la Kushughulikia viwanda vidogo vidogo (SIDO) ambalo tayari limeajiri wafanyakazi 160.

Alisema kuwa Shirika la Kushughulikia viwanda vidogo vidogo (SIDO) pamoja na majukumu mengine lakini lilikuwa na kazi mbili ambazo ni kuhakikisha wanatengeneza vipuli na mashine mbalimbali ambazo zimeharibika. Vileviele kuhamasisha wabanguaji wadogo wadogo na kuwasajili.

“Baada ya kuwasajili mtatakiwa kuingia nao mikataba kwa kiasi cha korosho wanachokihitaji kwa ajili ya ubanguaji” Alikaririwa Mhe Hasunga

Mhe Hasunga alisema kuwa serikali ina matumaini makubwa kuwa mikataba ya ubanguaji iliyosainiwa itazingatiwa kwa kufuata taratibu na masharti yote kwa mujibu wa sheria.

Alisisitiza kuwa serikali inaingia mikataba na viwanda ambavyo vimekuwa vikibangua kwa muda mrefu hivyo haina mashaka na ubora wa ubanguaji.

Aidha, Alisema kuwa viwanda hivyo vitakuwa na uhakika wa kufanya kazi usiku na mchana kutokana na malighafi nyingi iliyopo tofauti na miaka iliyopita ambapo malighafi ilikuwa haipatikani kutokana na korosho kubanguliwa nje ya nchi.

Mhe Hasunga amesisitiza kuwa serikali imeamua kubangua korosho zote nchini ili kuongeza wigo wa ajira kwa wananchi sambamba na kuongeza thamani ya korosho inayozalishwa nchini ili iweze kuuzwa kwa jina la Tanzania. Ambapo Wizara ya Kilimo itaweza kuchangia kwa ufasaha katika uchumi wa nchi.

MWISHO



from MPEKUZI

Comments