Waziri Mkuu Majaliwa Amwakilisha Rais Magufuli Katika Mazishi Ya Mke Wa Mufti Wa Tanzania

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amemuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli katika mazishi ya mke wa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakary Bin Zubeir yaliyofanyika Kwamndolwa, Korogwe mkoani Tanga.

Akitoa salam kwa niaba yake amesema “Rais Dkt. Magufuli aliweka nia ya dhati kushiriki mazishi haya ila kwa bahati mbaya leo ana mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika jijini Arusha ambapo yeye ni Mwenyekiti.”

“Mheshimiwa Rais amenituma nije nikupe pole wewe, watoto, familia na wote walioguswa na msiba huu. Mheshimiwa Rais anawaombea kwa Mungu ili mpate utulivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na nguzo katika familia. Haya yote ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu.”

Waziri Mkuu ameshiriki mazishi hayo ya mke wa Mufti, Bibi Hidaya Omar leo (Alhamisi, Januari 31, 2019).

Kadhalika, Waziri Mkuu amewasihi wafiwa na waombolezaji wote waendelee kuwa watulivu na kumuombea marehemu kila mmoja kwa imani yake ili Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema.

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum akizungumza kwa niaba ya familia amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kumtuma Waziri Mkuu amuwakilishe katika mazishi hayo. Pia amewashukuru watu wote waliojitokeza kwa ajili ya kuifariji familia kutokana na msiba walioupata.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo niWaziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo, Mhe. Salma Kikwete, Mhe. Hawa Ghasia, Mhe. Mary Chatanda ,Mhe. Mkuu wa Mkoa wa TangaMartine Shigelana Masheikh wa Mikoa.


from MPEKUZI

Comments