Waitara Azipiga Marufuku Shule binafsi kufukuza wanafunzi wasiolipa ada

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amepiga marufuku wanafunzi wa shule binafsi ambao hawajamaliza ada kusimamishwa au kufukuzwa shule.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Alhamisi Januari 10, 2019, jijini Dar es Salaam, Waitara amesema kuanzia kesho Ijumaa ataanza kupokea taarifa kutoka kwa katibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri na wadhibiti ubora wa shule ambazo zimewafukuza au kuwarudisha wanafunzi.

Amesema ni marufuku mwanafunzi kusimamishwa au kufukuzwa shule kwa sababu ya kutolipa ada bila kujali anasoma shule ya umma au binafsi.

Waitara amesema jambo jingine ambalo Serikali haikubaliani nalo ni la wazazi kulazimishwa kulipa ada kwa mkupuo na iwapo hawajafanya hivyo wanafunzi hawataendelea na masomo hata kama mwaka uliopita walifanya hivyo.

"Nina sms (ujumbe mfupi wa maandishi) nilizotumiwa na wazazi wa shule ambazo zimerudisha wanafunzi nyumbani kwa kukosa ada na malipo mengine ya kiholela kama vile kulazimishwa kununua sare za shule shuleni, for figer, rim na madaftari ya ganda gumu (counter book),” amesema Waitara.

“Nataka maofisa elimu, wakurugenzi na makatibu tarafa kwenda kwenye hizi shule (anazitaja shule) hadi kufikia kesho niwe na majibu yanayoonyesha kupatikana ufumbuzi."

Waitara pia amewataka wazazi ambao watoto wao wamerudishwa kwa ajili ya kutolipa au kukamilisha ada wafike kwenye ofisi alizozitaja au Tamisemi kwa ajili ya kupatiwa  ufumbuzi.



from MPEKUZI

Comments