Wahukumiwa Miaka 7 Jela Kwa Kuchezesha Upatu na utakatishaji fedha.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu Jones Moshi na James Gatuni, kulipa faini ya Sh milioni 204 au kwenda jela miaka saba kwa kosa la kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha.

Waliohukumiwa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Rifaro Africa Ltd, Jones Moshi (42) mkazi wa Mbezi Beach Dar es Salaam na Mkurugenzi mwenza wa Kampuni hiyo, James Gatuni (35) raia wa Kenya.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, alisema katika kosa la kwanza la utakatoshaji fedha watu kila mmoja anatakiwa kulipa faini ya Sh milioni mbili na endapo watashindwa kufanya hivyo watatakiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani.

Mashauri alisema katika shtaka la pili linalohusu utakatishaji fedha haramu kila mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 100 na endapo atashiwa kufanya hivyo atalazimika kutumikia kifungo cha miaka mitano jela.

“Lakini wakishindwa kulipa faini za makosa yote watatakiwa kutumikia kwenda gerezani kama adhabu kwa makosa yote mawili” alisema Mashauri.

Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, akisaidiana na Wakili Esther Martine na Neema Mbwana alidai mahakamani hapo kuwa wawili hao walitenda kosa hilo kati ya Julai 14 mwaka 2014 na March 31 mwaka 2016, jijini Dar es Salaam na maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


from MPEKUZI

Comments