Tamko La Wizara Ya Afya Kulaani Mauaji Ya Watoto 10 Mkoani Njombe

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inalaani na kukemea vikali vitendo vya mauaji ya watoto kumi (10) vilivyotokea katika wilaya ya Njombe ndani ya kipindi cha mwezi Desemba 2018 hadi Januari 2019; na hivyo kusababisha  taharuki kubwa kwa familia, jamii na Taifa kwa ujumla. Vitendo hivi havikubaliki kabisa katika jamii yetu na vinakiuka Sheria za nchi yetu.

Wizara inachukua nafasi hii kuzikumbusha familia zote katika jamii kuhakikisha zinaimarisha ulinzi na usalama wa watoto. Familia zinahimizwa kuwaangalia watoto na kujiridhisha wakati wote kuwa watoto wako wapi, wako na nani, wanacheza maeneo gani ili kuhakikisha wakati wote wanakuwa salama.

Aidha, Wizara inaikumbusha jamii na wazazi wote kwa ujumla kuzingatia jukumu la kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto ndani ya maeneo yao. 

Sheria ya Mtoto kifungu cha 95 inamtaka kila mwanajamii ambaye ana ushahidi au taarifa kwamba haki za mtoto zinakiukwa au ziko hatarini kukiukwa atoe taarifa mara moja kwa vyombo vya ulinzi na usalama katika eneo husika ili kuzuia uwezekano wa vitendo viovu kutokea. 

Hivyo Wizara inatoa wito kwa wanajamii wote na kamati za Ulinzi na Usalama wa Mtoto kuhakikisha wanachukua hatua haraka na kutoa taarifa katika vituo vya polisi, Ofisi za Serikali za Mitaa na Mamlaka husika.

Wizara inatoa rai kwa uongozi wa Halmashauri zote Mikoani kuendelea kuanzisha na kuimarisha Kamati za Ulinzi na Usalama wa Wanawake na Watoto. 

Wizara ina imani na inalishukuru kwa dhati Jeshi la Polisi mkoani Njombe kwa juhudi wanazofanya kuhakikisha inawatia nguvuni watuhumiwa wa mauaji haya na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Wizara inatoa pole kwa wazazi, walimu na ndugu wote walioguswa na msiba wa watoto wetu wapendwa, na kwa pamoja tunaomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.


from MPEKUZI

Comments