Tamko la Taasisi ya WAJIBU kuhusu sakata la Spika Ndugai, na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)

Taasisi ya Wajibu ambayo mkurugenzi wake ni Ludovick Utouh aliyewahi kuwa CAG imesema busara inahitajika kutumika ili kumaliza sintofahamu iliyopo kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

==>>Hapo chini kuna Tamko la Taasisi hiyo.
 
MAONI YA WAJIBU - INSTITUTE OF PUBLIC ACCOUNTABILITY JUU YA WITO WA SPIKA WA BUNGE KUMTAKA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI KUKUTANA NA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE 21/01/2019

WAJIBU - Institute of Public Accountability (WAJIBU), ni Taasisi inayojihusisha na masuala ya uwajibikaji hapa nchini. lmeendelea kufuatilia kupitia vyombo vya habari Tamko la Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kauli ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyoitoa kwenye mahojiano ya ldhaa ya Kiswahili ya Redio ya Umoja wa Mataifa (UN Redio).

Kwa kuwa suala hili limeleta sintofahamu kwa jamii,WAJIBU ikiwa ni miongoni mwa taasisi fikra za uwajibikaji nchini imeona ni vizuri itoe maoni huru kwa kuzingatia maslahi mapana katika uwajibikaji na utawala bora nchini. lfamike kuwa Bunge na CAG ni vyombo vinavyotambulika na kulindwa kikatiba.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), pamoja na Sheria ya Kinga, Haki na Mamlaka ya Bunge ya mwaka 1988, Bunge ni mhimili unaoishauri na kuisimamia Serikali katika matumizi bora ya rasilimali za umma. Kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge ya mwaka 1988 kinasema (tafsiri isiyo rasmi):

"Bunge, Kamati za Kudumu au Kamati za Muda za Bunge kulingana na matakwa ya kifungu cha 18 na kifungu cha 20 cha Sheria hii, zinaweza kuagiza mtu yeyote kuhudhuria mbele ya Bunge au Kamati husika kutoa ushahidi au kuwasilisha nyaraka alizonazo au zilizo chini ya usimamizi wake ".

Katiba hiyo hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 143 (1-5) pamoja na Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 zimeainisha majukumu ya CAG. Aidha, Ibara ya 143(6) inampa CAG kinga na uhuru wa kutoingiliwa na mtu au taasisi yeyote ya Serikalikama inavyonukuliwa hapa chini:

"Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2), (3) na (4) ya ibara hii, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yeyote au idara yoyote ya Serikali, lakini maelezo hayo ya ibara hii ndogo hayataizuia Mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo".


Kwa kuzingatia umuhimu wa taasisi hizi mbili katika kusimamia rasilimaliza umma na kukuza uwajibikaji na utawala bora, ni vyema busara ya hali ya juu itumike baina ya pande hizi mbili katika kutatua mgogoro huu kwa sababu dhana ya uwajibikaji na utawala bora nchini itaimarika iwapo tuu kutakuwepo na uhusiano mzuri kati ya taasisi zote za uwajibikaji na usimamizi nchini.

Kutokana na umuhimu wa Taasisi hizi mbili ambazo zinatakiwa kushirikiana kwa karibu sana katika kuimarisha uwajibikaji na utawala bora hapa nchini, wananchi wanashauriwa kutoa maoni yatakayoboresha na kuimarisha uhusiano wa taasisi hizi.

Kwa muktadha huo, WAJIBU inaamini kwamba sintofahamu iliyojitokeza kati ya CAG na Bunge nivyema ikashughulikiwa kwa busara kati ya pande zote mbili bila kuathiri uhuru wa kikatiba uliotolewa kwa Mhimili wa Bunge na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

lmetolewa na:
Bodi ya Wakurugenzi
WAJIBU - Institute of Public Accountability


from MPEKUZI

Comments