Taasisi Ya Moyo Ya Jakaya Kikwete Yawa Ya Kwanza Afrika Mashariki Na Kati Kuwa Na Wodi Ya Watoto Wenye Magonjwa Ya Moyo

Na: Genofeva Matemu – JKCI
Taasisi ya Moyo ya Jakaya kikwete (JKCI) imekuwa   taasisi ya kwanza Afrika Mashariki na Kati kuwa na wodi pekee ya kuwahudumia watoto wenye magonjwa ya moyo bila kuwachanganya na watu wazima.

Eneo la wodi hiyo lilitolewa mwaka 2017 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Magufuli alipokua akizindua Hospitali ya Mloganzila na kuiagiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutoa sehemu ya jengo linalohudumia watoto kwa JKCI ili watoto wenye magonjwa ya moyo waweze kuwa na wodi yao katika kuleta ufanisi wa matibabu ya moyo kwa watoto hapa nchini.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa wodi hiyo Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamaii, Jinsi, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alisema upatikanaji wa wodi hiyo ni juhudi za serikali katika kuhakikisha utolewaji wa matibabu ya moyo kwa watoto ya kibingwa yanaendelea kuboreshwa hapa nchini.

“Kwa wodi za watoto wenye magonjwa ya moyo peke yake kwa hapa Afrika Mashariki na kati hii ndio itakua wodi ya kwanza inayowahudumia watoto bila kuwachanganya na watu wazima na hii italeta ufanisi zaidi kwani nafasi ya kufanya makosa haitakuwepo kwasababu kutakuwa na wataalamu wanaohudumia watoto tu” alisema Waziri Ummy

Waziri Ummy, alisema  wodi hiyo ambayo ukarabati wake umekamilika inatarajiwa kuwa  na vitanda 32 na chumba cha uangalizi maalum (ICU) kitakachokuwa na vitanda 15 jambo ambalo litasaidia kuwafanyia upasuaji watoto wengi zaidi waliopo katika foleni ya upasuaji na kuokoa maisha yao.

“Serikali ilitoa milioni 700 kwa ajili ya ukarabati wa wodi hii na sasa kwa mara nyingine tena serikali imetoa milioni 500 kukamilisha miundombinu ya ukarabati wa wodi hii. Nawashukuru sana taasisi ya Baps Charity ambao nao wamewekeza  milioni 800 katika kuhakikisha kuwa wodi hii inakarabatiwa, serikali tutazidi kuunga mkono juhudi hizi ”  alisema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prf. Mohamed, Janabi alisema kwa shifti mbili za kliniki ya watoto zilizopo JKCI inaona wagonjwa wa moyo hadi sitini kwa siku thelathini wakiwa ni watoto, hivyo kulikuwa na umuhimu wa kuongeza wodi hiyo ya watoto.

Akizungumzia upasuaji wa magonjwa ya moyo prof. Janabi amesema kuwa jumla ya wangonjwa 1356 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na bila kufungua kifua kwa mwaka 2018, hii kwa mwaka jana ukiondoa Afrika kusini JKCI ndio hospitali iliyofanya upasuaji kwa wangonjwa wa moyo wengi zaidi kuliko nchi yoyote ya Afrika.

“Wodi hii mpya ni kwaajili ya watoto chini ya miaka 13 pekee na hii itatufanya kuwa taasisi ya kwanza Afrika Mashariki na kati kuwa na jengo lenye kuhudumia watoto bila kuwanchanganya na watu wazima “alisema prof. Janabi


from MPEKUZI

Comments