Taarifa Kwa Umma Kuhusu Mkutano Maalum Wa 38 Wa Baraza La Mawaziri EAC

Mkutano Maalum wa 38 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanyika jijini Arusha kwa lengo la kujadili na kukubabaliana na agenda mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 1 Februari, 2019.
 
Mkutano huo ambao unaongozwa na Mwenyekiti kutoka Jamhuri ya Uganda ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Kirunda Kivejinja utajadili agenda mbalimbali muhimu ambazo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taarifa kuhusu masuala ya miundombinu, forodha na biashara na ripoti ya kamati ya utawala na fedha.

Agenda zingine ni taarifa ya Baraza kwa Wakuu wa Nchi kuhusu utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yanayofiwa kwenye mikutano ya Wakuu hao wa Nchi na Kalenda ya Matukio ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni 2019.

Mkutano huo wa Mawaziri ulitanguliwa na vikao vya Maafisa Waandamizi kutoka nchi wanachama kilichofanyika tarehe 28 Januari kikifuatiwa na kikao cha Kamati ya Uratibu chini ya Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama kilichofanyika tarehe 29 Januri 2019.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo  unaongozwa na Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kuwahusisha pia Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), Waziri wa , Katiba
na Sheria, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), Waziri Fedha na Mipango, Mhe. Kapt. Mstaafu George Mkuchika (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mhe. Joseph Kakunda (Mb), Waziri wa Viwanda na Biashara na Mhe. Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa Kilimo.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inaundwa na nchi sita za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini imeendelea kuhakikisha wananchi katika nchi hizo wananufaika na Jumuiya hiyo hususan katika nyanja za biashara, ulinzi na usalama, viwanda, kilimo, miundombinu na huduma za kijamii.
 
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Arusha.
30 Januari 2019


from MPEKUZI

Comments