Kilichoendelea Leo Mahakamani Katika Kesi ya ESCROW inayomkabili Seth na Rugemarila

Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mfanyabiashara Herbinder Seth na James Rugemarila umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wapo katika hatua za kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo.

Hayo yameelezwa na Wakili wa Serikali (TAKUKURU), Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Swai amedai kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa, wapo katika hatua za kukamilisha upelelezi hivyo wanaomba tarehe nyingine.

Hata hivyo baada ya maelezo hayo, Wakili wa Utetezi, Dora Masaba aliuomba upande wa mashtaka wajitahidi kukamilisha upelelezi.

Pia wanaiomba upelelezi wa kesi hiyo ukamilike ili wajue mwisho wake ni nini kwani washtakiwa hao wapo gerezani tangu Julai 2017.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi February 14, 2019 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia upelelezi kama umekamilika au la.

Seth na mwenzake Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya dola za Marekani 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.


from MPEKUZI

Comments