Katibu Mkuu Madini Amsimamisha Kazi Afisa Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amemsimamisha kazi Fundi Sanifu wa Madini, Asheni Daudi wa Ofisi ya Madini Dodoma baada ya kuagizwa na Waziri wa Madini Doto Biteko.

Hatua hiyo ilifikiwa Januari 30, 2019, baada ya Waziri Biteko akiongozana na Katibu Mkuu na Wataalam wengine wa wizara vikiwemo Vyombo vya Ulinzi na Usalama, kufanya ziara ya kushtukiza katika Kiwanda cha Kuchenjua madini ya Dhahabu cha   Umoja kilichopo eneo la Viwanda la Kizota (Industrial Area) na kubaini mapungufu makubwa katika utendaji kazi wa wataalamu hususan uandaaji wa tarifa za uzalishaji wa madini.

Akizungumza katika eneo hilo, Waziri Biteko alisema wizara ilipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu mienendo inayoendelea katika eneo hilo ambapo wahusika ambao ni Maafisa Madini wamekuwa hawatoi taarifa halisi za uzito na ubora wa dhahabu zinazozalishwa baada ya kuchenjuliwa, hivyo, serikali kukosa mapato stahiki.

Waziri Biteko aliongeza kuwa, tayari anayo majina yote ya wanaofanya michezo ya ujanja ujanja kwenye viwanda vya kuchenjua dhahabu, huku akieleza kuwa, hatua madhubuti zitachukuliwa kwa wote wanaofanya vitendo hivyo na kuongeza kwamba, zoezi hilo litakuwa endelevu kwa lengo la kuwabaini wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuwataka maafisa madini kuwa makini.

Aidha, alimwagiza Kamishna wa Madini kufanya kaguzi katika viwanda vyote vya kuchenjua dhahabu kwa lengo la kubaini utendaji wa kazi wa viwanda hivyo, ikiwemo taarifa za uzalishaji zinazotolewa na kusema “Lazima tufike mahali tuheshimu taratibu, madini haya ni mali ya nchi”, alisisitiza Biteko.

Wakati huo huo, Waziri Biteko alimtaka Afisa Madini Mkoa wa Dodoma kujitathmini kutokana na mambo yanavyokwenda katika eneo lake la kazi na kumtaka kuwasilisha kwa Kamishna wa Madini na kwa Waziri wa Madini taarifa za uzalishaji madini ya dhahabu kwa kipindi cha miezi sita.

Pia, katika ziara yake, Waziri Biteko alibaini mnunuzi wa madini ya dhahabu katika eneo la Kizota aliyefahamika kwa jina la Matondo Michembe ambaye anafanya shughuli hizo bila kuwa na leseni ya biashara ya madini hayo. Hivyo, alimwagiza Michembe kuwasilisha taarifa za utendaji wake kwa Kamishna wa Madini na Waziri wa Madini hususan  soko analouzia madini hayo ya dhahabu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Prof. Simon Msanjila alieleza kuwa, kiutaratibu ilikuwa lazima taarifa za uzalishaji na kiasi kilichozalishwa kujazwa katika vitabu maalum ndani ya kiwanda hicho lakini jambo hilo halikufanyika kama inavyotakiwa.

Aliongeza kuwa, Afisa huyo amesimamishwa ili kupisha uchunguzi na endapo itabainika, taratibu za kiutumishi zitachukuliwa.


from MPEKUZI

Comments