EU yamtambua Mpinzani Juan Guaido kama rais wa Venezuela

Mgogoro wa kisiasa unaoendelea kuikabili Venezuela umechukua sura mpya Alhamisi mara baada ya bunge la Umoja wa Ulaya kutangaza kuwa linamtambua rasmi Juan Guaido wa Venezuela, kama rais wa muda wa nchi hiyo.

Bunge hilo limesema kuwa litaendelea kumtambua Guaido kama kiongozi wa Venezuela hadi pale nchi hiyo itakapofanya uchaguzi huru na wa haki. huku wajumbe 429 wakipiga kura kuunga mkono hatua hiyo wakati wa kikao maalum mjini Brussels, Ubelgiji.

Aidha, hatua hiyo, inaendelea kuongeza changamoto zinazomkabili rais Nicolas Maduro anayeegemea mlengo wa Kisocialisti, na ambaye anakabiliwa na mzozo mkubwa wa kisiasa tangu uchaguzi ulioibua utata mwaka jana.

Marekani na baadhi ya washirika wake wa Ulaya, zimetangaza pia kwamba zinamtambua Guaido, ambaye alikuwa kiongozi wa bunge la nchi hiyo, kama kaimu rais, hatua ambayo imepingwa vikali na Russia, China na Uturuki, kati ya nchi zingine, ambazo viongozi wao ni washirka wa karibu wa Nicholas Maduro.

Hata hivyo, wakati Venezuela ikiendelea kukabiliwa na migogoro ya kiuchumi na kisiasa, Umoja wa Ulaya tayari umeiwekea nchi hiyo vikwazo vya silaha na pia vya kibiashara, kuwazuia baadhi ya maafisa wa serikali ya Maduro kushirikiana kwa vyovyote vile na nchi wanachama wa muungano huo wa EU.


from MPEKUZI

Comments