Polisi Ahukumiwa Miaka 20 Jela au Faini Milioni 300

Polisi G.30 PC Reuben Mgamba (36) mkazi wa Forest jijini Mbeya amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka ishirini jela au kulipa faini ya Sh.Milioni 300 baada ya kukiri kukutwa na nyara za serikali meno ya tembo.
 
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Mbeya, Rashid Chaungu baada ya mshtakiwa huyo kufikishwa mahakamani na wenzake watatu wakidaiwa kuhujumu uchumi.
 
Akiwa mahakamani, askari huyo alikiri kukutwa na vipande vinne vya meno ya tembo jijini Mbeya kitendo ambacho ni kinyume na kifungu namba 86 (1) (2) (iii) cha sheria ya uhujumu uchumi Namba 5.
 
Awali akisoma shtaka hilo mahakamani hapo wakili wa serikali, Ofmedy Mtenga alidai, kwamba mshtakiwa huyo pamoja na wenzake watatu walikutwa na vipande hivyo katika eneo la Mafiati jijini hapa vyenye thamani ya Sh. Milioni 34,185,750.
 
Aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Askari Ex.G.30 Pc Reuben Mgamba James (36) mkazi wa forest jijini hapa, Safari Maneno (37) mfanyabiashara na mkazi wa Mabatini Mbeya, James Jeston Mnyamwezi (38) mkazi wa Namkukwe Mkoani Songwe na Adam Shaban maarufu kwa jina la Ilemu (40) mkulima na mkazi wa Mazimbwe wilayani Chunya.
 
Hata hivyo washtakiwa watatu wamekana kutenda kosa hilo licha ya mshtakiwa wa kwanza kukubali kukutwa na nyara hizo.
 
Wakili huyo wa serikali alieleza, upande wa mashtaka utawasilisha mahakamani ushahidi wake pamoja na vielelezo vya kuthibitisha shtaka hilo.
 
Aliiomba mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ambaye alikuwa mtumishi wa jeshi la polisi jijini hapa.
 
Hata hivyo baada ya polisi huyo kukiri kosa hakimu Chaungu
alimuamuru kulipa faini ya Shilingi milioni mia tatu au kwenda jela miaka 20 ikiwa atashindwa kulipa faini hiyo. 

Washtakiwa wengine watatu waliokana kutenda kosa hilo wamerudishwa mahabusu baada ya kukosa wadhamini hadi Januari 10, mwaka 2019 kwa ajili ya kuanza usikilizwaji wa kesi hiyo.


from MPEKUZI

Comments