Ndege za ATCL Zaanza Kuhujumiwa Na Wafanyakazi....Waziri Atoa ONYO

Naibu  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, amekemea tabia ya hujuma inayofanywa na baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya Ndege Tanzania-ATCL huku akikitaka kitengo cha masoko cha Kampuni hiyo kuhakikisha kinaangalia na kuondoa hujuma hizo.

Hujuma hiyo inatajwa kuwa ni ndege kusafiri bila kujaza abiria kwa manufaa ya ndege za mashirika mengine.

Naibu Waziri huyu alisema hayo jana wakati akifungua kikao cha tatu cha Baraza la Wafanyakazi wa ATCL, akisema hujuma hizo zinazofanywa na baadhi ya watoa huduma wa ndege hizo si nzuri na kwamba lengo la Serikali ni kuwekeza kwa Watanzania wote ambao utazaa matunda.

Alisema amekuwa akipokea simu kutoka maeneo mbalimbali kuwa ndege zinaondoka bila kujaa hasa za mikoa ya Kilimanjaro na Mbeya kutokana na baadhi ya watoa huduma hususan mawakala wa tiketi kuwa na tabia ya kuonwa na uongozi wa mashirika mengine ya ndege, hivyo kuacha kuuza tiketi za ATCL na kudai ndege imejaa na baadae ndege kuondoka na abiria pungufu.

“Baadhi ya mawakala huwa wanaonwa na viongozi wa ndege zingine na kudai ndege zao yaani ATCL zimejaa wakati hazijajaa ili ndege zingine zijae,” alifichua Nditite na kuongeza:

“Sasa najiuliza kwanini hawajali ajira na mshahara wao na kutegemea fedha za muda mchache, na hawana uzalendo na nchi yao, tunahitaji tija na sio hujuma.”

Aidha, alisema ATCL imepewa dhamana ya kuhudumia Watanzania wote na kwamba na ndege mpya zinatoa huduma nzuri, chakula na maji bure wakati ndege zingine hazifanyi hivyo.

Alisema, Serikali imeweka kipaumbele katika uendeshaji wa ATCL ambapo hadi sasa imeshapewa ndege nne ambazo ni Dash 8 Q400 tatu, Boeing 787 Dreamliner moja na hivi karibuni wanategemea kupeleka ndege nyingine mbili aina ya Airbus 220-300 huku wakitegemea kupokea ndege nyingine mpya ya Boeing 787 Dreamliner mwakani.

Hivyo alisema ni mategemeo ya Serikali kuona ATCL inafanya vizuri na kwa viwango vya kimataifa kwa kuwa ni fahari ya Tanzania.

Pia aliutaka uongozi wa ATCL kuimarisha kitengo cha biashara ili hujuma hizo zidhibitiwe mara moja.

Kadhalika, aliwataka viongozi na wafanyakazi kufanya kazi kwa weledi na bidii kubwa hasa katika kipindi hiki chenye changamoto nyingi na ushindani kibiashara kwa kuzingatia kutoa huduma bora, kuitii Serikali, kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa umma, kuheshimu sheria zilizopo na kutunza siri za Serikali.

Alisema ikiwa baraza hilo litazingatia kufanya kazi kwa weledi litaweza kwenda sambamba na soko lililopo ili uwekezaji wa Tanzania uliokusudiwa uweze kuzaa matunda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Ladislaus Matindi, alisema watahakikisha kitengo cha masoko na usalama wa ndani kinakuwa salama katika mifumo mbalimbali na kuendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri.

Matindi ambaye pia ni Mwenyekiti wa baraza hilo, alisema, mikakati ya shirika hilo ni kufanya biashara kwa kutoa huduma za kuvutia wasafiri.



from MPEKUZI

Comments