Kauli ya Zitto Kabwe Baada ya Rais Magufuli Kuamuru Kikokotoo cha Zamani Kitumike Mafao ya Wastaafu

Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe  amempongeza Rais John Magufuli kwa kukubali ushauri walioutoa na kuacha upande wa waziri, washauri wake na watendaji wa Serikali yake.

Maoni ya Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini ameyatoa leo baada ya Rais Magufuli kurejesha utaratibu wa awali wa kikokotoo cha asilimia 50 kwa watumishi wa Serikali na asilimia 25 kwa wafanyakazi wa sekta binafsi.

“Kufuatia uamuzi wa Rais Magufuli kuhusu kikokotoo cha mafao ya pensheni kwa wastaafu , sisi ACT Wazalendo na vyama vya upinzani kwa ujumla tumesimama na wafanyakazi toka mwanzo wa sakata hili, wakati sheria ikiwa muswada na hata baada ya kanuni kutungwa,” amesema 

“Kwetu, jambo lolote linaloongeza maslahi na ustawi wa wafanyakazi ni jambo jema na muhimu. Tunashukuru kuwa Mheshimiwa Rais ametuelewa na amekuja upande wetu na na kuacha upande wa waziri wake, washauri wake na watendaji wa Serikali yake,” ameongeza.

 “Tunapoelekea mbele, tunamuomba asiwe na aibu kutusikiliza na mengine mengi kwa kuwa  nia yetu  ni njema tunajenga nchi moja. Atusikilize na kuhusu mishahara ya watumishi wa umma atusikilize kuhusu mateso  ya wakulima wa korosho na atusikilize kuhusu sheria ya vyama vya siasa.”

“Kama hili la wafanyakazi hatukutumwa na mabeberu, basi na mengine pia hatutumwi na mabeberu,” amesema Zitto


from MPEKUZI

Comments