Deni la taifa Laongezeka Hadi Trilioni 49.37 kwa Mwaka 2018

Serikali  imesema deni la taifa limefikia Sh. trilioni 49.37 kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na Septemba 2017, lililokuwa Sh. trilioni 47.82 sawa na ongezeko la asilimia 3.2.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema hayo jana, wakati alipokuwa akitoa taarifa ya fedha ya hali ya uchumi wa taifa na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya nusu mwaka ya 2018/2019 iliyotolewa, jijini Dodoma.

"Nchi kuwa na deni sio dhambi, jambo muhimu ni kuhakikisha kuwa fedha tulizokopa zinatumika kujenga rasilimali ambazo ni msingi wa kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha mali na kulipa mikopo hiyo," alisema Dk. Mpango.

Dk. Mpango alisema, kufikia Septemba 2018, deni la taifa lilifikia kiasi cha Sh. trilioni 49.37, ikilinganishwa na deni hilo Septemba 2017, lililokuwa Sh. trilioni 47.82 sawa na ongezeko la asilimia 3.2.

Waziri Mpango alisema katika deni hilo, la ndani ni Sh. trilioni 13.64 sawa na asilimia 27.6 na la nje ni Sh. trilioni 35.72, sawa na asilimia 72.4.

Alitaja sababu za ndeni hilo kuwa ni mikopo ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam, ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, madaraja na bandari.

Sababu nyingine aliitaja kuwa ni ujenzi wa mitambo ya kufua umeme ya Ubungo, Mwanza na Kinyerezi II, miradi ya maji ikijumuisha wa maji wa Ziwa Victoria.

Alitaja sababu zingine kuwa ni miradi ya Tasaf, Mkongo wa Taifa wa mawasiliano na mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).

Hata hivyo, Dk. Mpango alisema matokeo ya awali ya tathmini iliyofanywa Desemba 2018, inaonyesha kuwa deni ni himilivu kwa muda mfupi na mrefu.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya mikopo, dhamana na misaada sura 134, serikali ina wajibu wa kufanya tathmini ya uhimilivu wa deni (DSA) kila mwaka ili kupima mwenendo wa deni na uhimilivu wake.

Katika tathmini hiyo viashiria vinaonyesha uwiano ufuatao: Deni la serikali kwa GDP asilimia 27.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 70.

Kwa uwiano wa deni la nje kwa GDP asilimia 22.2 ikilinganishwa na ukomo wasilimia 55, kwa deni hilo la nje mauzo nje asilimia 157.3, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 240 , ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa za nje asilimia 15.2 ikilinganishwa na ukomo asilimia 23 na ulipaji wa deni kwa mapato ya ndani ni asilimia 49.6.

Alisema viashiria vyote vinaonyesha kuwa serikali ina uwezo wa kuendelea kukopa na kulipa pale mikopo inapoiva.

Dk. Mpango alisema serikali itaendelea kusimamia deni na kuhakikisha kuwa linaendelea kuwa himilivu, mikopo itaelekezwa kugharamia miradi ya maendeleo yenye tija kwa taifa na ambayo inachochochea ukuaji wa uchumi.

Aliongeza kuwa serikali itaweka kipaumbele kukopa mikopo yenye masharti nafuu na kuhakikisha ya masharti ya kibiashara inakopwa kwa uangalifu mkubwa na inatumika kwenye maeneo yanayochochea ukuaji wa uchumi.

Aidha, alisema matarajio ya serikali ni kuwa viwanda vilivyojengwa na vitakavyojengwa vitachangia zaidi pato la taifa kwa kuchochea uzalishaji mali hasa bidhaa za kilimo.



from MPEKUZI

Comments