Bwana harusi afariki dunia akisubiri kufunga ndoa kanisani

Sherehe ya harusi iliyokuwa ifanyike juzi jioni katika Kanisa la Nabii wa Utukufu wa Bwana lilipo Olmatejoo, Kata ya Sakina jijini Arusha  kwenye ukumbi wa Sariko Olasiti Garden, iligeuka msiba baada ya bwana harusi kufariki dunia ghafla akiwa kanisani.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11 jioni katika kanisa hilo ambapo bwana harusi huyo, Heaven Makupa (47) alikuwa kanisani tangu saa saba mchana akisubiri kufunga ndoa na Jane Kimaro.

Hata hivyo, wakati sherehe, nderemo na vifijo vikiendelea vikiongozwa na kikundi cha matarumbeta nje ya kanisa huku bibi harusi akiingia kanisani, Heaven alianza kujisikia vibaya na kupoteza fahamu.

Kutokana na hali hiyo alikimbizwa Hospitali ya St Elizabeth, lakini alifikishwa akiwa tayari amefariki na mwili wake kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Mhudumu wa chumba hicho, Fransis Costa jana alikiri kuwa wanaendelea kuuhifadhi mwili wa bwana harusi huyo.

Ndoa hiyo ilikuwa ifungwe na kiongozi wa kanisa hilo, Nabii Peter Alayce na tayari taratibu zote zilikuwa zimekamilika tangu mchana alipofika bwana harusi na ujumbe wake.

Wakati kifo hicho kinatokea mamia ya watu walikuwa tayari wamefika katika ukumbi wa Sariko Olasiti Garden kuwasubiri maharusi hao ili kuendelea na sherehe.

Kutokana na tukio hilo, bibi harusi, Jane, alipatwa na mshtuko ambapo hadi jana baadhi ya ndugu zake ambao hawakupenda kuzungumzia msiba huo walisema alikuwa amepumzishwa.

Credit:Mwananchi


from MPEKUZI

Comments