Waziri Mkuu: Serikali Imejipanga Kumaliza Tatizo La Maji Nchini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa kuchimba visima virefu na vifupi pamoja na kutumia maji ya maziwa na mito na kuyapeleka katika maeneo mbalimbali ya wananchi nchini.
 
Pia, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wa wilaya kusimamia uhifadhi wa maeneo ambayo yana vyanzo vya maji ili kuyafanya yaendelee kuwa chepechepe, hivyo kuhakikisha vijiji vyote vinapata maji ya uhakika. “Lazima maeneo hayo yatambuliwe na yahifadhiwe.”

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Novemba 27, 2018) alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa shule Sekondari Bugando kata ya Nzera wilayani Geita, wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi za siku nne mkoani Geita.

Waziri Mkuu amesemaSerikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo yao ya makazi.

Amesema Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kila kijiji kinapata huduma ya maji safi na salama, hivyo amewaagizawatendaji wote wa vijiji kuainisha maeneo yote yenye misitu na vyanzo vya maji na kuhakikisha yanalindwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema mbali na huduma ya maji, pia Serikali imedhamiria kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo nchini vitaunganishiwa katika awamu ya tatu ya Mradi wa Nishati Vijijini (REA).

“Rais wetu Dkt. John Magufuli anataka kuona nyumba ya kila Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema  wananchi hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

Naye, Mbunge wa jimbo la Geita Vijijini, Joseph Musukuma ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi na ahadi zikiwemo na zile zilizotolewa za Rais Dkt. John Magufuli. “Nashukuru Serikali pia kwa kutuzindulia hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Geita.”

Kuhusu suala la umeme, Mbunge huyo ameishukuru Serikali kwa kuwa vijiji vyake vyote vimeshaunganishiwa umeme isipokuwa vitongoji vichache, ambapo ameomba navyo viunganishiwe nishati hiyo muhimu kwa maendeleo ya wananchi.

Awali,Waziri Mkuu alikagua na kuzindua hospitali ya wilaya ya Geita inayojengwa katika kata ya Nzera na aliupongeza uogozi wa halmashauri ya wilaya ya Geita kwa hatua waliyofikia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.


from MPEKUZI

Comments